Qasem Soleimani, Jenerali wa vikosi maalum vya Qudsi vinavyoungwa mkono na Iran, ameuawa na vikosi vya Marekani nchini Iraq.
Hayo yamejiri kufuatia ripoti ya mashambulio katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Baghdad, ambayo ilisema watu kadhaa wameuawa.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Javad Zarif, ametaja hatua hiyo kuwa "hatari na uchokozi wa kishenzi".
Katika Twitter yake Bw. Zarif aliandika: Marekani itawajibikia chochote kitakachotokana na hatua hiyo.
Gen. Soleimani alikuwa mtu mashuhuri kwa utawala wa Iran. Kikosi chake cha Qudsi kilikuwa kinaripoti moja kwa moja kwa kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei na alisifiwa kama shujaa wa kitaifa.
Rais wa Marekani Donald Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter picha ya bendera ya Marekani baada ya kutangazwa kuuawa kwa jenerali hiyo.
Ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zinasema kuwa Jenerali Soleimani na maafisa wa waasi wanaoungwa mkono na Iran nwalikuwa wakiondoka katika uwanja wa ndege wa Baghdad kwa kutumia magari mawili wakati waliposhambuliwa na ndege za Marekani zisizokuwa na rubani karibu na eneo kuweka mizigo.
Kamanda huyo aliripotiwa kusafiri kutoka Lebanon au Syria. makombora kadhaa yaliripotiwa kushambulia msafara wao, ambapo karibu watu watano wanaaminiwa kuawa.
Taarifa iliyotolewa na Pentagon ilisema: "Kufuatia agizo la rais, vikosi vya jeshi la Marekani vilichukua hatua ya kuwalinda wafanyikazi wake nje ya nchi kwa kumuua Qasem Soleimani,"
"Hatua hii ililenga kudhibiti mipango ya Iran ya mashabulio ya siku zijazo. Marekani itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuwalinda watu wetu na maslahi yetu kote duniani," ripoti hiyo iliendelea kusema.
Shambulio hilo la ndege zisizo na rubani linakuja baada ya siku kadhaa za maandamano ambapo waandamaanaji waliokuwa wakishambulia ubalozi wa Marekani mjini Baghdad kukabiliana na vikosi vya Marekani katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment