Adbox

Wednesday, February 26, 2020

Waathirika wa mafuriko Njinjo wahisi udanganyifu, waiomba serikali ichunguze

Na Ahmad Mmow, Lindi.

Baadhi ya waathirika wa mafuriko katika kijiji cha Njinjo, wilaya ya Kilwa wanahisi sehemu ya eneo lililotengwa na kijiji hicho kwa ajili ya viwanja vya makazi imeuzwa kinyemela. Kwahiyo wanaiomba serikali ichunguze ili kupata ukweli wa tetesi hizo.

Akizungumza kwaniaba ya wenzeke wenye mashaka hayo kwa sharti la kutotajwa jina lake kwa hofu ya kusumbuliwa na viongozi wanaoshukiwa kuuza eneo hilo alisema wanahofu sehemu ya eneo lililotengwa na kijiji hicho mwaka 2002 kwa ajili ya viwanja vya makazi ameuziwa mfugaji kinyemela. Kwani hakujaelezwa sababu za msingi za kutopimwa na kugawiwa wananchi eneo hilo ambalo ni tambarale na zuri kwa kujenga nyumba za makazi.

Alisema wanashangaa kuona viwanja vinapimwa kwenye mabonde wakati eneo hilo likiachwa. Lakini wananchi wanapouliza hawapewi majibu yanayoeleweka. Hata hivyo sababu za chini kwa chini zinatajwa kwamba eneo hilo ameuziwa mfugaji.

" Serikali iingilie kati, wapima walipokuja tuliwaomba watupimie na kule tukaambiwa eneo lile ni dogo na lipo mpakani na kijiji cha Miguruwe. Eneo la wazi. Mara kipimo cha GPRS kiliwaelekeza kule kwenye mabonde. Sasa sisi hatuelewi tu, hatusemi watu wote tupate kule. Watakaopata watapata, alimoradi lipimwe. Hapa mambo hayapo saw a, hata ng'ombe walitolewa na wafugaji kufuatia ombi la mkuu wetu wa Mkoa ili wachinjwe tupate kitoweo hawajulikani walipo," alisema.

Mwananchi huyo alisema wanatambua jitihada za serikali za kunusuru maisha yao. Jitiahada ambazo zinafanywa na serikali ya wilaya, Mkoa, taifa na wadau mbalimbali.Hata  hivyo shida ipo ngazi za chini. Hali ambayo inaweza kuvuruga jitihada na nia njema ya serikali dhidi yao iwapo haitadhibitiwa kikamilifu. Kwani baadhi ya misaada, ikiwamo vyakula vinakutwa kwa watu wasio sitahili. Ikiwa ni ushahidi kuwa baadhi ya viongozi wanaiba na kwenda kuficha kwa watu hao.

Diwani wa viti maalumu( CCM), Tabia Kiroboto alipoulizwa kuhusu malalamiko ya wananchi hao alisema hata yeye anayasikia yakizungumzwa na wananchi. Hata hivyo hawezi kusema ni kweli kama eneo linalotajwa kama limeuzwa. Kwani hakuna mwananchi aliyejitokeza na kutoa ushahidi kwamba limeuzwa nanani, lini, kwa nanani na kwabei gani. Bali kilichopo ni hisia tu.

Hata hivyo diwani huyo alisema tetesi hizo sio za kupuuzwa bali zifanyiwe Kazi. Akiweka wazi kwamba sababu zinazoelezwa za eneo hilo kutopimwa viwanja hazina uzito. Bali ataanza kuamini  hisia za wananchi nakuanza kufuatilia ili kujua sababu sahihi za eneo hilo kutopimwa viwanja iwapo zoezi la upimaji wa viwanja litakoma. Kwani zoezi la upimaji linaendelea.

Ofisa mtendaji wa kijiji hicho,Yahya Mketo alisema maelezo ya wananchi hao hayana ukweli na hofu yao haina msingi. Kwani eneo linalotajwa kutopimwa viwanja limetengwa kwa ajili ya shughuli za kijamii na taasisi za umma. Aliweka wazi kwamba tangu kuanza zoezi la upimaji hakuna mtu aliyejitokeza na kuwazuia wapimaji kwamadai ya kumiliki eneo.

Alisema yapo maeneo tofauti katika eneo lililotengwa. Kwasasa wanaendelea kupima kwenye eneo ambalo lilianza kupimwa viwanja na wataalamu wa idara ya ardhi. Lakini upo upande wa karibu na mnara wa kampuni ya simu ya airtel, ambalo litapimwa wakati wowote kuanzia sasa iwapo utapatikana muhafaka na wananchi wenye mashamba kwenye eneo hilo. Upande mwingine ni huo unaotajwa na wananchi.

Maelezo ya Mketo yanakaribiana kufanana na maelezo ya kaimu mkuu wa idara ya ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Kilwa, Ernest Mwakang'ata ambaye alisema hadi wanaondoka katika eneo hilo walishapima viwanja 528. Nakwamba upande uliopo mnara wa kampuni ya simu ya airtel walizuiwa na baadhi ya wananchi kwamadai kuna mashamba ya ufuta.

Alisema hakuna ukweli wowote kwamba GPRS iliwalazimisha wapime upande mmoja. Huku akiweka wazi kwamba wananchi wangeweka wazi sababu ya kuzuiwa na wenzao wachache wasipime eneo lililotajwa kuwa na mashamba wangekwenda kupima. Kwani wasingeogopa kupima kwasababu kuna mtu ameuziwa kinyemela. Lakini hawakuambiwa limeuzwa, bali lina mashamba.

Kuhusu kutengwa eneo kwa ajili ya shughuli za umma, Mwakang'ata alisema; " Mnapokuwa kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi lazima yatengwe maeneo hayo maalumu. Lazima tuainishe na kubainisha matumizi ya maeneo husika. Sasa sijajua eneo linalotajwa  limeuzwa ni lipi. Nidhahiri uchunguzi na ufuatiliaji unahitajika ili kupata ukweli,".

Alipoulizwa kama yupo tayari yeye na timu yake kwenda  Njinjo kujiridhisha. Alisema kazi ya kupima imeachwa kwa kamati ndogo ya ardhi huko kijijini, ambayo inaendelea na kazi. Hata hivyo wakihitajika watakwenda, iwapo taratibu zitafuatwa. Kwani ni wajibu wao wa msingj.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai alisema malalamiko ya wananchi hao hayawezi kupuuzwa. Hata hivyo kunahitajika umakini na utulivu mkubwa. Ili asionewe wala kulindwa yeyote kufuatia ufuatiliaji na uchunguzi utakaofanywa.

" Nakuhakikishia hakuna atayelindwa wala kuonewa, watu wote ni sawa mbele ya sheria . Awe mtendaji wa kijiji,mwenyekiti, of is a mtendaji wa kata hata governor( ofisa tarafa) ikibainika ni kweli, na ameshiriki kutenda yanayosemwa na wananchi atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Ngubiagai alisisitiza kwamba yeye kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi ya wilaya hiyo kwa kushirikiana na kutumia vyombo vya ulinzi  anaanza uchunguzi haraka ili kubaini ukweli wa hofu hiyo ya wananchi.

No comments:

Post a Comment

Adbox