Mwenyekiti wa Kitongoji cha kwa Mbwera Kijiji cha Kiwangwa wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Omary Koyo, amelalamikia tabia ya wakazi kulima na kujenga pasipokuacha eneo kwa ajili ya barabara.
Akizungumza na Mwandishi wa habari kitongojini hapa juzi, Koyo alisema kuwa wananchi katika eneo hilo wanalima mananasi wengine kujenga nyunba pasipokuacha eneo kwa ajili ya barabara, hali inayokwamisha maendeleo.
"Nimechaguliwa kushika nafasi hii kwenye uchaguzi uliomalizika hivi karibuni, moja ya changamoto niliyokutana nayo na naifanyiakazi ni ya ujenzi na namna wanavyolima mashamba ya mananasi, wanalima na kujenga pasipokuacha nafasi kwa ajilj ya barabara," alisema Koyo.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo hata zoezi la usambazaji wa nguzo za umeme kwenye eneo hilo limekuwa gumu, kutokana na wanaosambaza nguzo hizo kushindwa kupitisha hata tololi la kubeba nguzo, hivyo kulazimika kubeba mabegani hali inayosababisha usumbufu mkubwa.
"Kama kungekuwa na njia za uhakika za kupitika vizuri kazi ha kusambaza nguzo katika maeneo mbalimbali lingekuwa jepesi, lakini kutokana na ujenzi holela na ulima kumekuwa na ugumu kidogo utekelezaji wa kazi hiyo," alisema Mwenyekiti huyo.
Mmoja wa madereva wa magari yanayobeba mananasi kutoka mashambani akijitambulisha kwa jina la Rashid Jombo, alisema kuwa changamoto ya ufinyu wa barabara umekuwa adha kubwa katika eneo zima la Kiwangwa, kutokana na watu kulima mpaka barabarani.
"Suala la barabara eneo zima la Kiwangwa limekuwa na changamoto, watu wanalima mpaka jirani na barabara utakuta upande wa kulia na kushoto wanashindana kuibana barabara, magari hayawezi kupishana," alisema Jombo.
Aliongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo magari hayawezi kupishana kutokana na ufinyu huo, na kwamba dereva akimuona mwenzake anakuja mbele mmoja analazimika kutafuta eneo lenye nafasi asimame ili wapishane ndipo waendelee na safari.


No comments:
Post a Comment