Kutokana na uharibifu uliotokea,baadhi ya wakazi wa mji wa Mbinga wameiomba Serikali kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafikisha mahakamani makandarasi na wahandisi wa wakala wa barabara vijijini na mijini Tanzania (TARURA) kwa kushindwa kusimamia majukumu yao ikiwemo ujenzi wa mradi huo chini ya kiwango.
Walisema, ni kawaida baadhi ya barabara katika mji wa Mbinga kuharibika ndani ya muda mfupi tangu zinapojengwa na hali hiyo inatokana na wahandisi kushindwa kutumia taaluma zao wakati wa kutekeleza miradi ya Barabara katika wilaya hiyo.
Wamesema, kupeana kazi za ujenzi wa miradi ya barabara kwa misingi ya urafiki na kujuana kwa kiasi kikubwa kumechangia miradi mingi ya barabara katika mji huo kujengwa chini ya kiwango na hivyo kushindwa kuleta tija.
Aidha,wameiomba taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza mikataba inayoingiwa kati ya Tarura na Makandarasi ili kufahamu juu ya uwezo wa wakandarasi wanaopewa kazi katika Mji wa Mbinga.
Wakiongea kwa nyakati tofauti,wakazi hao Antonia Komba,Daud Shija na Suzana Ndomba wamesema, baadhi ya miradi inayojengwa haimalizi kero za wananchi licha ya kutekelezwa kwa fedha nyingi za walipa kodi wa nchi hii.
Antonia Komba mkazi wa mtaa huo, alitolea mfano ujenzi wa mifereji iliyojengwa katika barabara ya Kipika mtaa wa Kipika imedumu kwa miezi saba tu tangu ilipojengwa na sasa imeharibika kutokana na kusombwa na maji ya mvua na hivyo kushindwa kumaliza kero ya muda mrefu ya wananchi wa kata ya Matarawe.
Alisema, mifereji hiyo badala ya kuleta faraja kwa wananchi imeonekana sio salama hasa kwa watoto wadogo wanaopita maeneo hayo wakati mvua zinaponyesha ambapo maji kutoka maeneo ya milimani yanapita kwa wingi.
Mkazi mwingine Daud Shija amesikitishwa kuona mifereji iliyojengwa kwa fedha nyingi imeanza kuharibika kabla ya mvua hazijawa kubwa na hivyo kuwa na hofu kuhusu uwezo wa mkandarasi aliyejenga mifereji hiyo.
Shija ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la TAG Mbinga, ameiomba Serikali kupitia taasisi na idara zake kupima na kujiridhisha juu ya uwezo wa wakandarasi wanaoomba kazi za ujenzi ili kuepusha matumizi mabaya ya fedha za Serikali.
“kwa kweli nilipoona mifereji inajengwa katika eneo hili nilifurahi na kuipongeza sana Serikali kwa hatua hii,lakini furaha yangu imepotea ghafla baada ya kuona mifereji yote imeharibika kwa muda mfupi tangu ilipojengwa, mimi kama Mtanzania naishauri Serikali lazima iwe makini na waandisi wake na wakandarasi”alisema Mchungaji Shija.
Ditram Shabani alisema, uwezo mdogo wa makandarasi ndiyo sababu ya mifereji hiyo kuharibika kwa muda mfupi, tofauti na matarajio ya wakazi wa mtaa huo kwani ni kama hakufanya kazi yoyote katika eneo hilo ambalo ni kiungo muhimu kwa wakazi wa kata ya Matarawe na maeneo mengine ya Mji wa Mbinga.
Suzana Ndomba alisema, ‘’kila mvua inaponyesha maji yanayopita katika eneo hilo yanakuwa na kasi kubwa hali inayo hatarisha maisha ya watoto wadogo na hivyo wanalazimika kuwafungia ndani kama hatua ya kuwaepusha kusombwa na maji.
Meneja wa wakala wa Barabara(Tarura)Mji wa Mbinga Ismail Mafita hakupatikana kutolea ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi kwa kuwa yuko nje ya wilaya ya Mbinga na hata alipotafutwa kwa njia ya simu alikataa kujibu chochote badala yake alituma ujumbe mfupi (sms) yuko Hospitali.
Hata hivyo,Kaimu Meneja wa Tarura Amos Agustine alikiri kuharibika kwa mifereji iliyojengwa katika eneo hilo,ambapo alisema hali hiyo imetokana na athari za mvua zinazo endelea kunyesha kwa wingi katika wilaya ya Mbinga.
Amos ameitaja kampuni iliyojenga mifereji ni Stumack Engineering Co Ltd ya Dar es salaam huku akitaja gharama za mradi huo ni shilingi Milioni 33.6.
Kwa mujibu wake,kazi ya ujenzi wa mradi huo ilianza mwaka 2018 na kukamilika mwaka 2019 ambapo muda wa uangalizi umemalizika tangu tarehe 17 Novemba mwaka huu na mkandarasi ameshakabidhi mradi kwa Tarura.
Aidha alieleza,mpango uliopo kwa sasa ni kumpata mkandarasi mwingine ambaye atajenga upya mifereji hiyo, hata hivyo alisisitiza kuwa, suluhisho la kudumu ni kujenga barabara kwa kiwango cha lami katika eneo hilo sambamba na kuimarishwa kwa mifereji.
Alisema, eneo hilo ni kati ya maeneo mengi katika Mji wa Mbinga ambapo barabara zake zimeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika mji wa Mbinga.
Mkandarasi wa mradi huo aliyefahamika kwa jina moja la Mwafyenga alipotafutwa kwa njia ya simu alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sababu yuko Hospitalini amelazwa.
No comments:
Post a Comment