Adbox

Friday, January 3, 2020

Wafanyabiashara walalamika lugha chafu na vitisho kutoka kwa maofisa wa TRA

WAFANYABIASHARA mkoani Mbeya wamelalamikia maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwa wanawatolea lugha chafu na vitisho vinavyokuwa kikwazo kwao kulipa kodi kwa hiari.

Wakizungumza mbele ya Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, wafanyabiashara hao walimdai baadhi ya maofisa wa mamlaka hiyo mkoani Mbeya, wamekuwa wakitumia lugha kali kuwalazimisha kulipa kodi.

Walidai baadhi yao pia hawana ushirikiano kwa wafanyabiashara katika kutoa elimu kwa mlipakodi na kila kunapokuwa na kosa, hukimbilia kutoza faini bila kuwapa fursa ya kujitetea.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika maeneo ya Kabwe na Sido jijini Mbeya, Emmanuel Ndakam, alisema kauli za vitisho zimekuwa zikijenga ukuta na kuweka uadui kati ya wafanyabiashara na watumishi wa TRA, hali ambayo inakwamisha suala ulipaji kodi kwa hiari.

Ndaka aliuomba uongozi wa juu wa TRA kuwaelimisha watumishi wake ili kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara kwa lengo la kuboresha ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Alisema wafanyabiashara walio wengi, hawana uelewa na elimu ya kutosha kuhusiana na masuala ya kodi, hivyo bado wanahitaji elimu badala ya kupigwa adhabu kila wakati.

Alitoa mfano kuwa suala la wafanyabiashara kuandaa taarifa za biashara zao pamoja na elimu ya kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ni tatizo kwa wafanyabiashara walio wengi, hivyo wanahitaji kupewa elimu.

"Baadhi ya watumishi wa TRA ni kikwazo kwa wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari, mfanyabiashara anaweza kufanya kosa mfano kwenye suala la utoaji wa risiti, pengine kwa mashine ya EFD kukorofisha, badala ya ofisa wa TRA kumwelimisha, yeye anamtolea lugha za vitisho," alilalamika.

Edmund Msaki, mfanyabiashara katika eneo la Kabwe jijini hapa, alisema ziara ya mkurugenzi huyo kutoka makao makuu ya TRA inaonyesha wazi kuwa viongozi wa ngazi ya juu hawana tatizo, bali watendaji wao wa chini.

Alisema ujio wa kiongozi huyo wa ngazi ya juu utasaidia kuwapunguzia hofu wafanyabiashara wa Mkoa wa Mbeya ambao wakati wote wamekuwa wakiona TRA kama maadui.

Akijibu hoja za wafanyabiashara hao, Kayombo, aliyeongozana na maofisa wengine kutoka TRA Mkoa wa Mbeya, alisema lengo la kuwatembelea wafanyabiashara hao ni kutoa elimu na kusikiliza vikwazo vinavyowakabili.

Mkurugenzi huyo pia alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wafanyabiashara umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati.

Kayombo alisema wamekuwa wakiwapa elimu watumishi wa TRA namna ya kuwahudumia wateja na wamekuwa wakichukua hatua na kinidhamu dhidi ya walioonekana kwenda kinyume cha maadili.

"Lengo la ziara yetu ni kuwaona wafanyabiashara ili kusikiliza kero zenu, lakini kutoa elimu kuhusiana na masuala ya kodi na kuwakumbusha kulipa kodi kwa wakati pamoja na umuhimu wa kutoa risiti kwa wateja mnaowahudumia," alisema.

No comments:

Post a Comment

Adbox