Kutokana na wanafaika hao kushindwa kurudisha mikopo kwa wakati, baadhi ya wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo wameshindwa kupata mikopo hiyo.
Hayo yamo kwenye toleo maalum la Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18.
"Kutopatikana kwa wanufaika hao kunapunguza uwezo wa bodi kutoa mikopo kwa wanafunzi wapya na wanaoendelea," ilisema sehemu ya kitabu hicho katika ukurasa wa 42.
CAG alitoa mapendekezo kwa HESLB kushirikiana na taasisi nyingine na vyanzo vingine vya taarifa kuboresha kanzi data yake ili kuwatambua wanufaika wa mikopo ambao bado hawajatambulika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, kuhusu ukaguzi unaofanywa na ofisi yao, Mkaguzi kutoka Ofisi ya CAG, Henry Naiman, alisema eneo la mikopo ilibainika kuwa jambo hilo limekuwa kikwazo.
Alisema kutopatikana kwa wanufaika hao kumesababisha bodi hiyo kupunguza uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wapya na wale wanaoendelea.
"Ni vyema bodi hiyo ikashirikiana na taasisi nyingine lengo wanufaika wa mikopo wajulikane," alisisitiza Naiman katika kipengele hicho.
Mwishoni mwa mwezi Desemba, wanafunzi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ilitangaza mgomo kwa madai ya kutopewa mikopo tangu kufunguliwa kwa chuo hicho na kusababisha kuishi kwa tabu.
Siku chache baadaye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, alitoa onyo kali kwa wanafunzi hao waliotangaza mgomo na kuagiza uongozi wa UDSM kuchukua hatua.
Siku iliyofuata uongozi wa UDSM uliwasimamisha masomo wanafunzi na viongozi wa serikali ya wanafunzi ambao walidaiwa kuvunja kanuni za chuo hicho.
Pia serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), iliiomba serikali kuharakisha upatikanaji wa mikopo kwa kuwa wanaishi maisha magumu toka vyuo hivyo vifunguliwe.
Siku chache baadaye Bodi ya Mikopo ilitangaza kuanza kutoa fedha kwa wanafunzi walioko vyuoni, ikiwamo wanafunzi 698 walioshinda rufani mbalimbali.
MASHIRIKA 11 TAABANI
Katika ripoti hiyo ya CAG, pia ilionyesha kuwa mashirika ya umma 11 yanajiendesha kwa hasara kwa zaidi miaka miwili na kuwa tegemezi kwa msaada kutoka serikalini.
Kwa mujibu wa Mkaguzi Naiman, mashirika hayo yanajiendesha kwa hasara tofauti na mashirika mengine.
MENGINE 14 YASUASUA
Alisema mashirika 14 ya umma yana changamoto za kifedha na kupata hasara ambayo inawasababishia madeni kuwa zaidi ya mitaji yao.
Ripoti hiyo ilitoa mapendekezo kwa serikali ifanye mapitio ya namna ya uendeshaji wa mashirika hayo na kuongeza mitaji ili yaweze kumudu gharama za uendeshaji.
Kadhalika ripoti hiyo ilionyesha kuwapo kwa wadaiwa sugu wa pango jumla ya wapangaji 623 wanaoendelea kupokea huduma ya upangaji katika kituo cha mikutano cha AICC licha ya kuwa na madeni sugu yanayofikia Sh. bilioni 3.8.
NIC YAELEMEWA
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Shirika la Bima la Taifa (NIC) limeripotiwa madai ya kiasi cha Sh. bilioni 53 wakati deni halisi ni Sh. bilioni 63 madeni hayo yana upungufu wa thamani halisi ya kiasi cha Sh. bilioni 10.
"Kuna uwezekano kuwa mapato yaliyorekodiwa hayakuwa halisi hivyo serikali imependekeza mashirika halisi yanatakiwa kutekeleza sera zao za upangaji na usimamizi wa madeni ili kuwa na usimamizi imara wa mapato," ilisema ripoti hiyo.
Alisema wakifanya hivyo watagawanyika kwa kiasi kikubwa kuwa na mifumo imara ya usimamizi wa mapato ya fedha ambazo zinatakiwa kupatikana.
No comments:
Post a Comment