Adbox

Thursday, November 21, 2019

Rais Magufuli avitaka vyuo kufanya tafiti zinazonufaisha Jamii

Na. Ezekiel Mtonyole, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli, amevitaka vyuo  hapa nchini kujikita kufanya utafiti mbalimbali ambazo zitakuja na suluhisho la kutatua Changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii zetu.

Pia amevitaka vyuo hivyo vitafute mbinu ya kuhakikisha  vinazalisha watimu wanaoweza kujiajiri na sio kutegemea kuajiliwa na umma.

Dkt. John Magufuli ameyasema hayo leo Jijini Dodoma katika maafali ya kumi(10) ya Chuo Kikuu Cha Dodoma, UDOM, ambapo pia ametunukiwa Shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa, katika chuo hicho, ambapo wahitimu takribani elfu sita(6000) watatunukiwa Shahada mbalimbali.

Dkt. Magufuli amesema vyuo vinawajibu wa kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitasaidia kuja na suruhisho la kutatua changamoto mbalimbali katika jamii .

"Vyuo vyetu hivi vijitahidi kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitasaidia Jamii hasa katika kilimo, ufugaji na viwanda na pia uchimbaji wa madini, tafiti hizo ziwasaidie wakulima, namna ya kufaidika na shughuri zao"

"Pia vyuo hivi vijikite katika kuzalisha wahitimu ambao wataweza kujiajiri na sio kuzalisha wahitimu wa kuja kuajiriwa na Umma, na ninyi wahitimu mkawe Chachu katika kuziondoa changamoto zilizopo katika jamii na sio ninyi kwenda kuwa changamoto katika jamii" amesema Dkt Magufuli.

Aidha amesisitiza kwa serikali na taasisi mbalimbali mbali kujenga Utamaduni wa kutumia wataalamu wanaozalishwa ndani ya nchi, ili kupunguza gharama kubwa na kupunguza wasomi ambao wamehitimu na hawana kazi ya kufanya.

Pia ameelezea mafanikio ambayo yamepatikana katika awamu ya tano, kuwa serikali imefanya Mambo mengi ikiwamo, ununuzi wa ndege, upanuzi wa viwanja vya Ndege, na ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege msalato ambao itawezesha ndege yoyote duniani kutua.

Ameongeza kuwa mengine,ni "Kubana matumizi kwa serikali, kuondoa watumishi hewa, kuzuia safari za nje ya nchi, kukarabati shule kongwe na vyuo vya ufundi, pamoja na kuongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu, na kutoa elimu bure" amesema.

Mbali na mafanikio hayo amesema zipo changamoto ambazo  zinajaribu kukwamisha juhudi hizo kuwa ni mabeberu, vibaraka wa ndani na nje ya nchi ambao wanajaribu kukwamisha juhudi hazo na kusema hawata kata tamaa na wataendelea kuwatumikia wananchi.

No comments:

Post a Comment

Adbox