Adbox

Thursday, November 21, 2019

Mkopo wa Bilioni 8 kujenga kituo kipya cha Mabasi

Na Paschal Malulu-Kahama

Serikali ya halmashauri ya mji wa Kahama wilayani Kahama mkoani Shinyanga inatarajiwa kukopa mkopo wa shilingi bilioni nane katika benki ya TIB BANK kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani (NEW MBULU BUS TERMINAL).

Imeelezwa kuwa kituo hicho cha mabasi kitakuwa cha kisasa ambacho kitakuwa ni moja ya chanzo cha uingizaji mapato ya ndani ya halmashauri hivyo kituo hicho kinatarajiwa kujengwa eneo la Mbulu mjini humo chenye ukubwa wa hekta za mraba 4.60.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kahama Clemence Mkusa amesema utekelezaji wa ujenzi huo halmashauri iliandaa nyaraka mbalimbali kwa kushirikiana na wataalam washauri ikiwemo ya kuwasilisha michoro na makadirio ya gharama za ujenzi (BOQ), mahitaji ya msingi ya kutafuta fedha na nyaraka za zabuni.

Mkusa amesema baada ya wataalam hao kukamilisha na kuwasilisha kazi zao halmashauri ya mji ilipeleka nyaraka hizo katika benki ya TIB, shirika la nyumba la taifa (NHC) na OR-TAMISEMI kwa lengo la kupata fedha ambazo zilifanyiwa kazi na kurejeshwa kwa wataalam kwa marekebisho ya mwisho.

Amesema mradi huo ulipendekezwa kutumia vyanzo vikuu vya ruzuku na mkopo na wakati ukiendelea serikali kupitia wizara ya fedha ilisitisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa fedha za ruzuku hivyo mradi huo ulisimama huku akiongeza kuwa baraza la madiwani kupitia vikao vyake tayari limekubali halmashauri ya mji kuchukua mkopo huo wa bilioni nane.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Kahama mjini kupitia chama chama mapinduzi (CCM) Hamidu Kapama amesema kituo hicho kitakuwa chanzo muhimu hivyo wao kama madiwani wamekubali na halmashauri ianze mara moja utekelezaji kwani kwa sasa kituo cha mabasi kilichopo hakitoshi kwa mahitaji ya magari.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Kahama ambaye ni diwani wa Kata ya Nyasubi kupitia chama cha mapinduzi Abel Shija amemtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhakikisha mkopo unachukuliwa haraka ili utekelezaji wa mradi uanze.

No comments:

Post a Comment

Adbox