Adbox

Saturday, November 2, 2019

Naibu Waziri Ikupa asisitiza matumizi ya lugha za alama katika mikutano vyama vya siasa

Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Stella Ikupa, amevihimiza vyama vya siasa kote hapa nchini kuhakikisha wanawatumia wataalamu wa lugha ya alama katika mikutano yao kutafsiri ili kuwawezesha walemavu wa kusikia kuelewa kinachoendelea kwenye mikutano hiyo.

Naibu Waziri Stella ameyasema hayo  Jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la kuwajengea uwezo wawakilishi wa watu wenye ulemavu katika kushiriki katika uchaguzi wa serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 ya mwezi huu.

Amesema vyama vyote vya siasa hapa nchini vione haja ya kutumia wataalamu wa lugha za alama katika mikutano yao ili walemavu wa kusikia nao wawe na uwezo wa kuelewa mambo yanayoendelea katika mikutano hiyo ili nao wasiachwe nyuma hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.

"Hata katika ziara zangu maeneo mbalimbali huwa natoa maelekezo kwenye halmashauri mbalimbali nimekuwa nikisisitiza watu watumie wataalamu wa lugha ya alama, hata kwenye mikutano ya vyama vya siasa nashuri watumie na lugha ya alama"

"Kwenye shughuli zao yani hapa mlemavu wa kusikia unamwambia aende kwenye kupiga kura anafika pale hajui mgombea kasema nini au kanadi Sera gani kwahiyo ni muhimu Sana vyama vya siasa watumie wataalamu wa lugha angalau na hawa wajue nini kinaendelea na mgombea kanadi sera gani" amesema Naibu Waziri Stella.

Aidha amesema angalau hata watu wenye ulemavu mbalimbali inapofikia kwenye vipindi vya uchaguzi walemavu wapate habari zinazohusu uchaguzi sawa na watu wengine wasiokuwa na ulemavu.

Amevitaka vyama vya siasa kuzingatia sheria ya vyama vya siasa kwa kuweka utaratibu ili hata watu wenye ulemavu nao waweze kushiriki katika michakato mbalimbali ya vyama vya siasa hapa nchini sambamba na kutumia madhaifu ya chaguzi zilizopita ili yasijirudie katika uchaguzi huu.

Amesema walemavu nao wasikubali kubaki nyuma katika maswala ya uongozi, hasa wahakikishe waingia katika vyama vya siasa ili nao wawe miongoni mwa watu wanaochaguliwa kupitia vyama hivyo na hatimaye kupata uongozi kupitia vyama hivyo na vyama navyo vimetakiwa kutowaacha nyuma walemavu katika teuzi zao.

Pia amewataka walemavu watakaofanikiwa kuchaguliwa wakawe mfano kwa kufanya kazi kwa bidii ili weendelee kuaminiwa na wengine waendelee kupata nafasi katika ngazi mbalimbali, pia amewataka kutumia mkutano huo kubadilishana mawazo na njia bora ya kushiriki katika uchaguzi ujao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa SHIVYAWATA taifa Ummy Nderiananga, amesema Kongamano hilo ni la siku mbili kwa ajili ya kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu katika kushiriki katika chaguzi zijazo hasa katika uchaguzi wa serikali za Mitaa na hatimaye kugombea hata katika uchaguzi Mkuu mwakani.

Aidha amebainisha kuwa kama chama cha walemavu SHIVYAWATA  kimepewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa mikoa 15, hivyo wamepongeza hatua hiyo kuwa ni kuaminiwa kwa chama hicho na wataendelea kushirikiana kwa Mambo mbalimbali na kufanya kwa uaminifu.

"Kongamano hili limeandaliwa na kituo cha Sheria na haki za binadamu, na ni la siku mbili linalengo la kuhakikisha watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika maswala ya uchaguzi, pia katika hali ya kuonekana chama kinaaminiwa tumepewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa mikoa 15 hii ni faraja kwetu" amesema Ummy.

Amewapongeza wabunge na Madiwani ambao walithubutu na kujiingiza katika kuwania nafasi na hatimaye kupata, akiwamo Naibu Waziri Stella Ikupa, na kuwataka watu wenye ulemavu kuiga ujasili huo kwa kujiingiza kugombea nafasi mbalimbali katika vyama vya siasa na katika uchaguzi.

Nae Mratibu katika Ofisi ya kituo Cha sheria na haki za binadamu(LHRC) William Mtwazi, amesema wamekuwa wakishiriki Kati Ujenzi wa taifa na hasa katika kutetea haki za minadamu na wamekuwa karibu na jamii katika kutetea haki za binadamu kote hapa nchini kwa kutoa msaada wa kisheria na wamekuwa wakishirikiana vizuri na Serikali hasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Naye mmoja wa washiriki wa Kongamano hilo ambaye ni Katibu wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulimavu Mkoa wa Dodoma, Jastas Ng'wantalima, amesema Kongamano hilo ni la umuhimu Sana kwao kwani hapo mwanzo walikuwa wameachwa nyuma Sana katika maswala ya uchaguzi Sasa semina Kama hii itakuwa na manufaa makubwa kwao katika kushiriki katika uchaguzi huu.

No comments:

Post a Comment

Adbox