Adbox

Tuesday, November 26, 2019

CCM kuaendelea kutambua na kuthamini mchango wa wazee wa chama hicho

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk Bashiru Ali amesema chama cha Mapinduzi  kinaendelea kuwatambua na kuthamini mchango na juhudi mbali mbali zilizofanywa na wazee wa chama hicho katika mapambano ya kujenga na kustawisha Taifa.

Amesema  wazee wamefanya kazi kubwa  na wanaendelea kufanya kazi kuhakikisha kuwa amani ya nchi inaendelea kudumu, hivyo ni vyema kuendelea kuthamini mchango wao ndani ya chama.

Kauli hiyo leo  wakati akizungumza na wazee mashughuli wa chama cha Mapinduzi, katika ukumbi wa ofisi kuu ya CCM, Zanzibar Kisiwandui mjini Zanzibar.

Alisema wazee hao wanakumbukwa kwa mchango wao na unathaminiwa na kuendelea kuenziwa hasa kwa Chama cha Mapinduzi kwani hawafanyi hivyo kwa kujipendekeza bali ni wajibu wao.

"Nyinyi wazee mnastahili kuthaminiwa kusikilizwa na kuenziwa na sisi tuna wajibu wa kufanya hivyo na tusipofanya hivyo basi tutafuta laana," alisema.

Akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika katika vitongoji, kata na mashina Dk Bashiru alisema CCM imeshinda katika uchaguzi huo kwa asilimia 99.

Hivyo alisema, matokeo ya ushindi huo inaonesha dhahiri kwamba CCM ni chama kinachoendelea kukubalika kwa umma na kuona kinajiandaa vyema katika kuhakikisha kinashinda katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Aidha aliwaomba wanaCCM kujiandaa kuona kila mara wanapitia mikakati yao, mbinu zao, ahadi zao ambazo wamekuwa wakizitoa baada ya mapambano ya ukombozi wa uhuru na enzi za Afro Shirazi na TANU ili waendelee kuwa chama kinachoaminika kwa umma kuongoza serikali zote mbili.

Hata hivyo alisema ushindi huo ni mtaji mkubwa hivyo imefika wakati kutojibweteka,kutoridhika na kujiamini kupindukia bali ni kufanya tathmini ya kuona maeneo yenye nguvu zaidi kuendelea kuyaimarisha na yale yenye udhaifu kusahihisha udhaifu huo.

Sambamba na hayo aliwaomba wazee kuendelea kuwa mfano bora kwa wale ambao wamepewa dhamana kwa kuwarithisha tabia njema, kuwashauri na kuwapa busara na hekima na pale wanapokosea kuwaelekeza ili waweze kujisahihisha.

"Mafanikio tunayoyapata sisi viongozi wa sasa ni matunda yanayotokana na jasho lenu nyinyi wazee wakati mkiwa katika majukumu mbalimbali ndani ya serikali na chama chetu," alisema.

Katika maelezo yake Dk, Bashiru alisema, hivi sasa chama kinaendelea na mabadiliko makubwa kimfumo, kimuuondo na kitaasisi kwa kuendelea kuunda mabaraza ya wazee na kuyaahuisha kwani yameonekana kutetereka.

Alisema agizo lilotolewa na Halmashauri kuu ni kuyaimarisha mabaraza ya wazee kupitia viongozi katika ngazi zote kwani mabaraza hayo ni muhimu sana kwa chama.

Katibu huyo mkuu alisema, agizo jengine ni kuimarisha demokrasia katika ngazi ya mashina kwa mabalozi na wenyeviti wa mashina ili kutambuliwa mchango wao kuhakikisha kila nyumba ya balozi na mwenyekiti wa shina inakuwa na bendera ya chama.

Lakini pia aliendelea na kusema kuwa sambamba hayo alikini piamabalozi hao watapatiwa kitambulisho ambacho kitamuwezesha kuingia katika tasisi mbalimbali za serikali kwa ajili ya kueleza kero za wananchi ambao wanawaongoza.

Kwa upande wake Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa, Kombo Hassan Juma alisema wazee hao wamepambana na wanaendelea kupambana na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa huru na CCM inabaki madarakani.

Alisema, wazee hawa wanaendelea kutoa mchango mkubwa sana katika Chama cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla kuhakikisha kuwa chama kinaendelea kuwa imara.

Naye Mwenyekiti wa Wazee wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Khadija Jabir alisema, wao kama wazee wamejiandaa vizuri katika kuhakikisha kuwa ushindi wa kishindo unapatikana katika uchaguzi wa mkuu wa 2020.

No comments:

Post a Comment

Adbox