Adbox

Friday, October 18, 2019

Wanafunzi vyuo vikuu waanza kupata mikopo

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeanza rasmi kutoa mikopo kwa wanafunzi na kutangaza orodha ya awamu ya kwanza yenye wanafunzi 30,675 wa mwaka wa kwanza wa masomo 2019/2020 waliopata mikopo yenye thamani ya Sh. Bilioni 113.5.

Tayari katika bajeti ya mwaka huu, serikali ilitenga Sh. Bilioni 450 zitakazowanufaisha wanafunzi 128,285 kati yao, zaidi ya 45,000 ni wa mwaka wa kwanza na wengine 83,285 ni wenye mikopo wanaoendelea na masomo.

Akizungumza na wanahabari Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Abdul- Razaq Badru alisema pamoja na awamu hiyo ya kwanza awamu nyingine ya wanafunzi iliyobakia itatangazwa kupatiwa mikopo yao kabla ya mwisho wa wiki ijayo.

"Hawa tutajumuisha na wale wengine waliobaki ambao tumewapa muda wa kurekebisha taarifa zao na fedha zao zitatumwa vyuoni mapema kabla ya vyuo havijafunguliwa," alisisitiza.

"Hawa wanafunzi 30,675 tumejiridhisha na vigezo na fedha zao tayari tunazo kesho (leo) tunaanza kuzisambaza kwa vyuo husika kwa kuwa serikali imeshatukabidhi Sh bilioni 125 tulizoomba kwa malipo ya kati ya Oktoba hadi Desemba, mwaka huu," alisema Badru.

Alisema kati ya wanafunzi hao wa awamu ya kwanza, makundi maalumu yenye uhitaji yamepewa kipaumbele ambao ni wanafunzi 6,142 yatima au waliopoteza mzazi mmoja, wanafunzi wenye ulemavu 280 na wanaotoka kwenye kaya zinazofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) 277.

No comments:

Post a Comment

Adbox