Adbox

Friday, October 18, 2019

Katibu Mkuu Wizara ya Afya asisitiza mahusiano bora baina ya watumishi sekta ya afya

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula amezidi kusisitiza mahusiano bora baina ya watumishi walio katika sekta ya afya katika maeneo yao ya kazi na kuwataka kuongeza mapato ili yaweze kuendesha Hospitali na vituo vya afya pamoja na kuboresha hali za watumishi kwa ujumla.

Dkt. Chaula amesema hayo wakati akiendelea na ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa baada ya leo kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Misungwi Jijini Mwanza na kuona hali ya ujenzi wa jengo la huduma za uzazi na kuonekana kuridhishwa na ujenzi huo kisha kuongea na watumishi.

Katibu Mkuu huyo amesema lengo la kutembelea maeneo ya utoaji wa huduma za afya kanda ya ziwa ni pamoja na kuona maendeleo ya utoaji huduma na kuongea na watumishi ili kubaini maendeleo na kupata changamoto zinazowakabili na kuona namna gani ya kuzitatua.

Pamoja na yote yaliyozungumzwa Dkt. Chaula amewaomba watumishi hao kupendana na kufanya kazi kwa moyo ili kuwahudumia wagonjwa wanaofika kupata huduma huku akiwataka kuongeza mapato na kuweza kujilipa motisha kutokana na ufanyaji kazi wao.

Kabla ya hapo Dkt. Chaula alitembelea kituo cha afya cha Buzuruga na kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella katika uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya chanjo za Surua na Ribella kwa watoto wadogo nchini iliyozinduliwa kitaifa Mkoani Morogoro na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.

Badae Dkt. Chaula akiongozana na Wakurugenzi na viongozi waandamizi kutoka wizara ya afya na ofisi ya Rais TAMISEMI alitembelea ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Ilemela na kituo cha matibabu ya magonjwa ya hatari na milipuko (Isolation Highly Infectious Unit) cha Buswelu.

No comments:

Post a Comment

Adbox