Adbox

Wednesday, October 30, 2019

Ufuatiliaji na tathmini serikalini ni chachu ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma

Matumizi sahihi ya Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini Serikalini yanaongeza uwajibikaji na kuboresha utendaji kazi wa viongozi na watumishi wa umma nchini hivyo kuwa na mchango katika
maendeleo ya utumishi wa umma na taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati akifungua mafunzo ya wadau ya siku mbili yenye lengo la kuwajengea uwezo wa Ufuatiliaji na Tathmini watendaji wa Serikali yanayofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Michael amesema, kutokana na umuhimu wa Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini katika kuboresha nidhamu ya utendaji kazi Serikalini, kuna haja ya mfumo huo kuwepo kisheria ili utekelezwe kwa mujibu wa sheria katika Taasisi zote za umma nchini, hivyo kikao hiki kina jukumu la kutoa mapendekezo sahihi ya kutekeleza azma hiyo.

Dkt. Michael amefafanua kuwa, pamoja na kuanzisha sehemu za Ufuatiliaji na Tathmini kwenye Wizara, Idara Zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, ni muhimu
kwa viongozi wenye dhamana kuwa na utashi wa kisiasa katika kujenga Mfumo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ili kuongeza uwajibikaji serikalini.

Dkt. Michael ameongeza kuwa, Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini unatakiwa umguse mtumishi mmoja mmoja na taasisi kwa ujumla ambapo watumishi na taasisi hawana budi kuonyesha matokeo
chanya kulingana na rasilimali zilizopo na kwa upande mwingine, wananchi wana haki ya kuiwajibisha Serikali kwa kuitaka ionyeshe matokeo chanya katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa “Centre for Learning on Evaluation and Results CLEAR-AA” kutoka Chuo cha Witwatersrand nchini Afrika Kusini, Prof. Dugan Fraser amesema, kituo hicho kipo
tayari kushirikiana na Serikali katika kuwezesha matumizi sahihi ya Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini yatakayosaidia kuboresha uwajibikaji, utoaji wa huduma bora, kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati na kuimarisha Utawala Bora kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Aidha, Prof. Fraser amesikitishwa na baadhi ya watendaji wanaotumia muda mrefu kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali na kutoa taarifa za miradi hiyo kwa kuchelewa na
kusababisha taarifa zilizopatikana kutokuwa na mchango tarajiwa katika kufanya maamuzi.

Prof. Fraser ameweka bayana kuwa nchi isiyotumia Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini katika utekelezaji wa miradi yake husababisha kuwa na sera mbovu, wananchi kutopata haki ya kuishauri serikali au kutoa maoni juu ya utekelezaji wa miradi, na serikali husika kutekeleza programu za maendeleo bila ufanisi.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uchambuzi na Ushauri wa Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Nolasco Kipanda amesema kufanyika kwa semina
kunatokana na jitihada zinazofanywa na Serikali kuwajengea uwezo kiutendaji wataalamu wake wa ufuatiliaji na tathmini, hivyo amewataka wataalamu hao kutumia fursa hiyo kuongeza ujuzi ili wawe na tija kwa maendeleo ya taifa.

Semina hiyo ina lengo la kuwajengea uwezo wataalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini inahudhuriwa na wadau kutoka katika Wizara, Idara Zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa, Mahakama, Bunge, Tanzania Evaluation Association (TanEA) na washirika kutoka Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment

Adbox