Adbox

Sunday, October 27, 2019

TADCOS LTD yahimiza vyama vya ushirika wa mazao kushirikiana

Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.

Vyama vya ushirika wa mazao vimetakiwa kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha mbegu, mbolea na viwatilifu vinawafikia kwa wakati wakulima waliopo pembezoni hasa maeneo ya vijijini.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na mwenyekiti wa chama Cha wasambazaji wa pembejeo za kilimo na mifugo hapa nchini (TADCOS LTD), Gerard Mlenge, wakati Akizungumza na Muungwana Blog kuhusiana na changamoto wanazokutana nazo wakulima kwa kutopata pembejeo kwa wakati.

Amesema ili kuhakikisha wakulima wote waliopo vijijini wanapata mbolea na mbegu bora kwa wakati ni lazima ushirikiano uwepo baina ya vyama vya ushirika vya mazao ambavyo kila chama kinajua maeneo ambayo wakulima wanapatikana kulingana na zao wanalolima na msimu wa mvua katika ukanda waliopo.

"Naamini TADCOS LTD na vyama vingine vya ushirika tukishirikiana tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya upatikanaji mbegu bora kwa wakulima waliopo pembezoni mwa miji hususani vijiji vya ndani ambapo hawapati pembe jeo kwa wakati," amesema Mlenge.

Akizungumza kwa furaha Mara baada ya kupokelewa kwenye vyama na kuwa mwanachama kamili wa shirikisho la vyama vya ushirika, amesema wameamua kufanya hivyo lengo ni kutaka kuhakikisha wakulima waliopo vijijini wanafikiwa kwa wakati na mbegu bora ambazo husambazwa na TADCOS LTD kupitia vyama vya ushirika vya mazao.

Amebainisha kuwa lengo lao kama TADCOS ni kuona wakulima wanafaidika na kazi inayofanywa na Chama hicho hasa ukizingatia hivi sasa wakulima wanahitaji kufanya Kilimo chenye tija ambacho kitawanufaisha wao,jamii, na taifa kwa ujumla.

Amesema TADCOS inatarajia kuingia mkataba na kampuni zinazozalisha mbolea nje ya nchi ili kuboresha na  kurahisisha upatikanaji wa mbolea kwa wingi hapa nchini.

Kwa upande wake  Katibu wa TADCOS LTD,  Eliah Kajuni amewatoa wasiwasi wakulima  dhidi ya upatikanaji wa mbolea kwa sababu wanatarajia kuleta mbolea tani 45,000 kwa ajili ya msimu ujao wa Kilimo.

"Naomba wakulima wasiwe na wasiwasi mbolea itawafikia kwa wakati katika maeneo tofauti kulingana na msimu wa mazao wanayotarajia kupanda," amesema Kajuni.

No comments:

Post a Comment

Adbox