Adbox

Saturday, October 26, 2019

Mkuu wa Shule iliyofanya vizuri Kitaifa Matokeo kidato cha sita aanzishiwa Timbwili,asema haogopi

Na John Walter-Manyara

Uongozi wa shule ya Sekondari Dareda iliyopo wilaya ya Babati mkoa wa Manyara,imeshangazwa na wakaguzi wanaokuja kila mara shuleni hapo bila kujua ni kitu gani wanakikagua huku wakitoa Vitisho.


Akizungumza katika mahafali ya 25 ya Kidato cha nne mwalimu Mkuu wa shule hiyo Joel Laiza amesema anashangaa kuona wakaguzi wakimfuata mara kwa mara shuleni hapo bila kujua ni kitu gani wanakagua , lakini shule ilipokuwa ikifanya vibaya hakuwahi kuona wakaguzi wakifika kukagua, hivyo anashangaa kuwaona baada ya kusikia shule imefanya vizuri katika Matokeo Kitaifa.

“Hawa wakaguzi sielewi wanachokagua,yaani wananifuata mara kwa mara na kunitisha” alisema Laiza.

Amesema hayupo tayari kuona wanafunzi wanapata ziro kwa ajili ya uzembe wa walimu au wazazi hivyo wanaomtishia kwamba watamchongea kwa waziri waende wala haogopi.

“Wananipiga vita sana na wengine wanasema wataenda kwa waziri na waende,kama naye waziri atataka wanafunzi wasifanye vizuri aniambie ukweli sifai,mimi sina tatizo,division one zipo za kutosha hakuna Zero,nitazidi kusimamia Taaluma katika shule ya Sekondari Dareda”alisisitiza Mwalimu Laiza.

Mkuu huyo  amesema katika uongozi wake kwa kipindi alichosimamia taaluma amefanikiwa kuiweka shule hiyo katika sura mpya yenye mafanikio.

Naye Mgeni Rasmi katika Mahafali hayo Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi  (NEC) mkoa wa Manyara Joachim Mungano alimtaka  mkuu huyo wa shule aendelee kuchapa kazi bila kuwahofia  hao wanaomtishia na kwamba wataishia kupiga kelele kwani serikali ya Magufuli inaangalia wacahapa kazi na sio propaganda zisizo na mashiko.

 “Shule hii imetuweka katika nafasi nzuri kimkoa na hata kitaifa, kwani mwaka 2018 shule hii ilishika nafasi ya 14 kati ya shule 98 za mkoa huu pia kushika nafasi ya 624 kati ya shule 3488 kitaifa tofauti na miaka kadhaa ya nyuma”alisema.

Aliwataka walimu waongeze bidii waliyoionyesha kwa vitendo na kwamba kufanya hivyo ni kuunga mkono kauli ya Rais Dkt. John Magufuli ya hapa kazi tu.

Katika hatua nyingine Mjumbe wa Halmashauri kuu Taifa NEC mkoa wa Manyara Joachim Mungano amefanikiwa kuchanga Jumla ya Tsh. 2,500,000/  papo kwa papo na wazazi waliohudhuria kwenye Mahafali hayo ili kuondoa kero iliyotajwa na wanafunzi hao kwenye risala yao ya kukosa mashine ya kutolea nakala (photo copy).

Alidai kuwa ni vema kuwatekelezea mahitaji yao ya muhimu kama walivyoainisha kwenye risala yao na kuwataka wazazi walioguswa na juhudi za walimu na wanafunzi  wajitokeze na kuwachangia wapate hiyo mshine ili kupunguza kero zilizopo.

Shule ya Sekondari Dareda ni Miongoni mwa shule za Serikali ambazo zina rekodi ya kufanya vizuri kitaifa katika matokeo ya kidato cha Sita mwaka jana ambapo iliingia katika shule bora 20

No comments:

Post a Comment

Adbox