Adbox

Friday, October 18, 2019

Kamishna Sabas afanya doria ya anga maeneo yaliyokumbwa na mafuriko

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo CP Liberatus Sabas, amefanya doria ya angani katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kuangalia maeneo ambayo yamekumbwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa siku za hivi karibuni.

Kamishna Sabas amesema kuwa, madhara yaliyotokana na mvua hizo ni madogo ambapo maeneo ambayo makazi ya watu yamezungukwa zaidi na maji ni maeneo ya Jangwani jijini Dar es Salaam sehemu ambayo tatizo hilo hutokea mara kwa mara licha ya wakazi wa maeneo hayo kuamriwa
kuhama kwenye maeneo hayo.

Aidha Kamishna Sabas ameongeza kuwa katika maeneo ya Kimara kumeripotiwa tukio moja la mtoto kufariki dunia jana baada ya kutumbukia kwenye mkondo wa maji na juhudi za kutafuta mwili wake zinaendelea.

Katika Mkoa wa Pwani watu takribani 17 wameokolewa jana kutoka maeneo hatarishi na kwenda maeneo salama ili kunusuru maisha yao. Pia Kamishna Sabas ametoa angalizo kwa wakazi wote nchini wanaoishi maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko wahame na kwenda maeneo ambayo ni salama ili kuepukana na madhara ya mvua.

Katika hatua nyingine Kamishna Sabas ametoa wito kwa Watanzania ambao bado hawajajiandikisha katika daftari la mpiga kura, kujiandikisha ili kuweza kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha uchaguzi huo
unafanyika kwa amani kuanzia katika kampeni mpaka uchaguzi wenyewe.

No comments:

Post a Comment

Adbox