Adbox

Thursday, October 24, 2019

Epukeni matumizi ya dawa zinazotangazwa mitandaoni - Waziri Ummy

Serikali imewataka wananchi kuepuka matumizi ya dawa zinazotangazwa kupitia mitandao ya kijamii kwa kuwa hazijadhibitishwa ubora wake na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Akizungumza Jijini Dodoma mara baada ya kikao  cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa kumekuwa na wimbi la watu mbalimbali  wanaotoa kiholela matangazo ya kuuza dawa za aina mbalimbali kupitia mitandao husika.

"Jamii itambue kuwa  kuuza dawa  ambazo hazijazidhitishwa ni kosa kisheria na niwatake wahusika kuacha mara moja kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao,”Alisisitiza Mhe Ummy.

Akifafanua, Ummy amesema kuwa ifahamike kuwa dawa siyo kama nguo,viatu ama bidhaa nyingine kama hizo ambazo mtumiaji anaweza kununua kadiri utakavyo kutokana na mahitaji  au uwezo wake, lakini dawa isiyothibitishwa na mamlaka ni sumu na kwamba inaweza kumgharimu maisha mtumiaji anayetumia bila maelekezo ama ushauri wa daktari.

Aliongeza kuwa,  Kamati hiyo imeitaka Wizara yake kuongeza jitihada katika kuzuia matangazo yanayotolewa kupitia mitandao ya kijamii yakinadi dawa  za aina mbalimbali ikiwemo kuhusu masuala ya uzazi na magonjwa mengine.

Aidha Ummy Mwalimu,amesema, tayari Wizara yake imeshaanza kuchukua hatua kupambana na vitendo vya kutangaza dawa na chakula mitandaoni bila kusajiliwa na kwamba tayari mtu mmoja ameshakamatwa na wakati wowote anatarajiwa kufikishwa mahakamani kufutia kitendo chake cha kutangaza dawa ya kuongeza viungo vya wanaume na kudai kuwa Waziri Ummy,alifungua duka husika lililoko Kariakoo,jijini Dar Es Salaam wakati taarifa hizo zikiwa si za kweli.

Katika hatua nyingine, aliwataka wale wote wanaotaka kuuza dawa kufuata taratibu zilizowekwa kisheria kuepuka kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo Oktoba 23, 2019 Bungeni Jijini Dodoma  imepokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

No comments:

Post a Comment

Adbox