Adbox

Sunday, September 1, 2019

Zanzibar bado ina fursa nyinyi za uchumi, vijana changamkieni''

MKUU wa wilaya wa Kusini Unguja Idrissa Mustafa amewataka vijana nchini kuchangamkia Fursa za kiuchumi zilizopo visiwani Zanzibar kwa lengo la kujiajiri na kutengeneza fursa za ajira kwa vijana wengine.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa Zanzibar bado ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo zikitumiwa ipasavyo itazalisha ajira nyingi kwa vijana.

Hayo aliyaeleza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib Unguja  wakati wa ufunguzi wa Kongamano la vijana kuhusu fursa za kiuchumi zilizopo visiwani Zanzibar,

Kongamano hilo limeandaliwa na Taasisi ya Itifaki, Upatanishi na Huduma za Kijamii Zanzibar na kufanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakili Kikwajuni Zanzibar.

Mkuu huyo aliwaeleza vijana hao kuwa wanatakiwa kuchangamkia fursa mbali mbali za kiuchumi zilizopo visiwani Zanzibar ili kujiinua kiuchumi kwa kujiajiri na kutengeneza fursa za Ajira kwa vijana wengine.

  “ Vijana ndio nguvu kazi ya Taifa katika kuinua uchumi nchini hivyo ni lazima mjikite katika kujituma wenyewe ili waweze kujipatia kipato cha halali,”alisema Mkuu wa Wilaya.

 Amewataka vijana kizitumia fursa ziliopo katika kujiajiri wenyewe kwa kufanya kazi mbali mbali zenye kuwapatia rizki na kuacha kusubiria ajira kutoka Serikalini ikiwa Serikali haiwezi kuajiri vijana wote.

 Aidha alisema ili vijana wawe na mustakabali mzuri wa  kukuza uchumi ndani ya nchi  na  kujiendeleza maisha yao   lazima wawe na elimu,wajiepushe na madawa ya kulevya ili Taifa liweze kuwa na  vijana wenye  afya bora na kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi .

“Elimu ndio ufunguo wa maisha hivyo itumieni elimu kwa kuifanyia kazi mbali mbali ikiwemo ujasiriamali kilimo na sio kuweka vyeti ndani na kusubiri ajira wakati unakupiteni”, alisema Idrissa.

Akitoa wito kwa vijana  kuwataka kuhakikisha kongamano hilo litawajengea uwezo na wakitoka hapo waweze kubadilika kwa kuibua mambo mengi katika kujiongezea kipato chao.

 Idrissa amewataka vijana kuacha  kufikiria kwamba utalii ni kutembeza wageni tu ila kuna kazi nyingi ambazo ni za utamaduni wetu  ujasiriamali tukizifanya watalii watavutiwa nazo na pato litaingia nchini.

Nae Dkt Miraji Ussi Mkurugenzi Masoko Kamisheni ya Utalii   amesema Zanzibar utalii unakuwa   miradi mingi ipo ya kuvutia watalii ikiwemo spice, kusuka mikeka na mambo mengine vijana wafanye kazi hizo ili  kukuza uchumi.

Pia amesema  miradi mingine ni sekta ya malazi, bangaloo,  na michezo ya ngoma za kiasili  na mambo mengi ya Wazanzibar ambapo watalii huvutika nayo na kuwaomba vijana wachangamkie fursa hizo.

Wakitoa michango katika kongamano hilo Siti Hussein Jumamwanafunzi kutoka Skuli ya Benmbela  aliiomba Kamisheni ya Utalii kuwapangia sera maalum watalii wanapoingia nchini kuhusu suala la kivazi ili utamaduni wetu wetu uweze kuimarika .

Kongamano hilo la siku moja mada nne ziliwasilishwa ikiwemo Ujasiriamali , Uchumi  sekta ya utalii, uchumi wa visiwani,na uchumi mafuta na gesi na kauli mbiu ya Kongamano hilo “TUMIA ELIMU KUWA FURSA YA MAENDELEO YA KIUCHUMI”

No comments:

Post a Comment

Adbox