Adbox

Monday, September 23, 2019

Waziri Mkuu afungua Maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa  hapo jana alifungua Maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji  kwenye Sekta ya Madini  yaliyoanza tarehe 20 Septemba, 2019 na kutarajiwa kumalizika tarehe 29 Septemba, 2019.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Waziri Mkuu Majaliwa ametoa  pongezi kwa Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa kuboresha shughuli za madini kupitia kuongeza ajira na  vitendea kazi kama vile magari kama njia mojawapo ya kuboresha ukusanyaji wa maduhuli.

Akielezea mafanikio ya Soko la Madini Geita tangu kuanzishwa kwake Majaliwa amesema kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa dhahabu kutoka takribani kilo 100 hadi kilo 200 na zaidi kwa mwezi na kusisitiza kuwa, tangu kuanzishwa kwa soko la madini la Geita kiasi cha kilo 1,573 zimezalishwa na kuuzwa.

Katika hatua nyingine, ameitaka Tume ya Madini kuongeza kasi kwenye ukusanyaji wa maduhuli ili Sekta ya Madini iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi .

Aidha, amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuyatumia vyema masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini na  kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha yanalindwa.

Pia, amewataka wachimbaji wa madini kutumia tafiti zinazofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) kubaini maeneo yanye madini na kuanza kuchimba ili kuepuka uchimbaji wa kubahatisha.

Amesema serikali itaendelea kuboresha Sheria na Kanuni ili kuleta tija zaidi  na hivyo kuwataka wananchi kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya madini ikiwemo kutoa taarifa kwenye vyombo vya udhibiti.

No comments:

Post a Comment

Adbox