Na Felix Mwagara, Katavi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka wananchi wa mikoa ya mipakani nchini kutoa taarifa za wahamiaji haramu ili kudhibiti matukio ya ujambazi na utekaji katika maeneo hayo.
Lugola alisema uhalifu katika mikoa hiyo licha ya kuwa imethibitiwa kwa kiasi kikubwa lakini bado baadhi ya mikoa ukiwemo Mkoa wa Katavi, wahalifu hutumia njia zisizo rasmi kuingia nchini na kufanya matukio ya uhalifu.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ikola, wilayani Tanganyika, Katavi, waziri Lugola aliwataka wananchi hao kutoa taarifa kwa vyombo vya dola, kwa mtu au watu ambao wanawatilia mashaka ili kudhibiti matukio mbalimbali ya uhalifu.
"Mnapaswa kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa za wahamiaji haramu katika maeneo yenu ili kuisaidia serikali yenu kuwasambaratisha wahamiaji haramu ambao wanafanya uhalifu wakishirikiana na Watanzania wasio waaminifu waishio mipakani, hii haiwezekani, na kamwe Serikali haiwezi kuchezewa," alisema Lugola.
"Wahamiaji haramu wapo mitaani kwetu, na mnawajua, hivyo mnapaswa kutoa taarifa kwa maafisa uhamiaji, Jeshi la Polisi au vyombo vingine vya dola nchini, ili Serikali ya Dkt. Magufuli iweze kuwatia mbaroni haraka iwezekanavyo," ameongeza.
Aidha, Lugola aliwataka Polisi kuwasaka na kuwakamata majambazi na kuwasambaratisha bila uwoga wowote maana mhalifu hawezi kuchekewa.
Kwa upande wake, Afisa Uhamiaji wa mkoa huo, Kamishna Msaidizi, Vicent Haule alikiri kuwepo na changamoto hiyo, na kuahidi kuwasaka wahamiaji haramu kupitia vyanzo vyote vya uchunguzi.
Haule alisema maeneo ya mipakani yana changamoto licha ya kuwa ofisi yake inafanya kazi usiku na mchana kupambana na wahamiaji haramu, na wapo tayari kupokea taarifa za wahamiaji hao watakapopewa na wananchi.
“Tunamshukuru sana mheshimiwa Waziri kwa kutupa maelekezo mbalimbali, hasa ya kuhusu masuala ya wahamiaji haramu, na uraia hasa pale makazi ya Katumba na Mishamo, kwasababu amewataka wakazi waliopewa uraia wasivunje sheria za nchi kwa kwenda Burundi na kurudi nchini bila kufuata sheria,” alisema Haule.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Lilian Matinga, alimshukuru Waziri Lugola kwa kufika katika wilaya hiyo na kuahidi maagizo yote aliyoyatoa kwa Wilaya hiyo watayafanyia kazi kupitia vikao vyao vya kamati ya ulinzi na usalama.


No comments:
Post a Comment