Adbox

Monday, September 2, 2019

Watumishi wa mafunzo ya Agro Studies Mjini Jerusalem watunukiwa vyeti

Jerusalem-Israel Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Japhet Hasunga leo,Septemba 2,  2019 ameshiriki mahafali ya mafunzo ya Kilimo ya Agro Studies yanayofanyika mjini Jerusalem nchini Israel na kuwatunuku vyeti vya kuhitimu wanafunzi 45 kutoka Tanzania.

Katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa ICC (Jerusalem International Conventional Center), Waziri Hasunga amewapongeza vijana hao kwa kuhitimu masomo yao hivyo amewaahidi kuwa serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imejipanga kuboresha mazingira wezeshi kwenye sekta ya kilimo hivyo wanayo nafasi nzuri kuutumia ujuzi walioupata kuboresha kilimo watakaporejea nchini Tanzania.

Mahafali hayo yatajumuisha vijana 1600 kutoka mataifa zaidi ya 12 ambapo kati ya hao vijana 45 ni watanzania, miongoni mwao wanawake wakiwa ni 9 na wanaume ni 36.

Waziri huyo wa kilimo wa Tanzania, Japhet Hasunga amesema kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepewa jumla ya nafasi 100 kwa ajili ya kupeleka vijana wa kitanzania kujifunza kilimo cha kisasa nchini Israel hivyo fursa hiyo ni muhimu kwani vijana hao wa Tanzania
wamepata ujuzi wanachotakiwa kufanya  ni kutumia ujuzi huo kwa manufaa makubwa nchini mwao.

Akizungumza mara baada ya kuwakabidhi vyeti wahitimu hao Mhe Hasunga amesema kuwa kupatikana kwa nafasi hizo 100 ni kutokana na ombi la Rais wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe
Magufuli kwa serikali ya Israel ili kuwawezesha vijana wengi wa kitanzania kujifunza mbinu na teknolojia za kilimo cha kisasa.

Kadhalika, Waziri Hasunga atakutana na kurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Agro Studies ambapo miongoni mwa mazungumzo muhimu itakuwa ni pamoja na kumuomba uwezekano wa kuongezewa nafasi zaidi ili vijana wengi wa kitanzania waende kujifunza mbinu mpya za kilimo nchini Israel.

Pia, Mhe Hasunga atakutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo nchini Israel kujadiliana nae maeneo mbalimbali na fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.

Katika mkutano mwingine, Mhe Hasunga atakutana na kufanya mazungumzo na wadau wawekezaji wakubwa wa sekta ya kilimo nchini Israel ili kuwaeleza fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Adbox