Adbox

Monday, September 23, 2019

Polepole awashukia vikali wanachama wa CCM wanaowania nafasi hii

Katibu, Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole amemfagilia Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya kuwa ni mchapakazi na anayewajibika kwa wananchi.

Hata hivyo, Polepole amewashukia vikali baadhi ya wanachama na makada wa CCM wanaoiwania nafasi hiyo ili hali mbunge wa jimbo hilo Ole Millya (CCM) anaendelea na nafasi hiyo.

Polepole ameyasema hayo kwenye kongamano la Simanjiro ya kijani lililofanyika Kata ya Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani na kuandaliwa na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Simanjiro.

Amesema Ole Millya ni kijana mwenye nguvu hivyo viongozi wa CCM na wa serikali wa wilaya ya Simanjiro wanapaswa kumpa ushirikiano wa kutosha ili wawatumikie wananchi.

“Tumekubaliana kwenye vikao vikubwa vya chama kuwa mahali palipo na mbunge wa CCM hapaswi kubuguziwa wala kuguswa na mtu yeyote wala hata wale wa CCM waache unyemelezi,” alisema Polepole.

Pia, amewakemea vikali baadhi ya viongozi wa CCM wa wilaya hiyo wenye siasa chafu ambao wanataka kumkwamisha Ole Millya katika nafasi hiyo.

“Hivi sasa tuna mbunge mmoja jimbo la Simanjiro naye ni Ole Millya, anapaswa kuachiwa nafasi hiyo kwani atatekeleza ilani ya CCM kwenye eneo hilo hivyo apewe nafasi afanye kazi yake,” alisema Polepole.

Amemtaka Ole Millya afanye kazi yake kwa uadilifu kwa kuwatumikia bila wasiwasi wowote wananchi wa Simanjiro ambao wana kiu kubwa ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Adbox