Na Ezekiel Mtonyole, Mpwapwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri amewataka wataalamu wa malisho kutoka halmashauri mbalimbali hapa nchini, kutoa elimu kwa wafugaji ili kuwajengea uwezo wa kutambua matumizi bora na endelevu ya nyanda za malisho.
DC Shekimweri amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya wataalamu na wadau wa malisho nchini yaliyofanyika katika chuo cha Mifugo Lita kilichopo Mpwapwa huku akiongeza kuwa utunzaji malisho ni muhimu kwa wafugaji kwa sababu itawasaidia kujua nini wanatakiwa kufanya ili kudhibiti uhaba wa malisho pale unapotokea.
Pia DC huyo ameongeza kuwa lengo lao ni kuona maafisa ugani hao wanatumia nafasi walionayo kutoa elimu hiyo kiufanisi kwa wafugaji katika halmashauri mbalimbali wanazotoka ambayo itasaidia kupunguza migogoro baina ya wafugaji na wakulima kugombea maeneo ya malisho.
"Mafunzo mliyoyapata mkayatoe kwa wafugaji katika sehemu mnazotoka tumieni nafasi yenu ili kuisaidia serikali ya awamu ya tano kuboresha sekta ya Mifugo," amesema Shekimweri.
"Mnapaswa kuhamasisha na kuongeza uvunaji wa malisho na matumizi ya teknolojia rahisi za kukata,kufunga,na kuhifadhi majani na masalia ya mazao ili yatumike wakati wa uhaba" amesisitiza.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo ya Ugani Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt Angello Mwilawa amesema uzalishaji wa malisho bora ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na mahitaji makubwa ya lishe bora na uhakika kwa Mifugo sambamba na ongezeko la mahitaji makubwa ya nyama na maziwa nchini.
Ameongeza Wizara imekuwa ikitekeleza moja ya mikakati yake wa upatikanaji wa uhakika wa malisho na Maji kwa Mifugo kwa kuilekeza jamii jinsi ya utunzaji wa maeneo ya malisho bira kwa mifugo.
"Wizara kwa kushirikiana na halmashauri nchini tumeanzisha mashamba ya mfano ya malisho bora ambayo yanalenga kuwajengea uwezo wafugaji wote nchini kuzalisha malisho bora katika maeneo yao," amesema Dkt Mwilawa.


No comments:
Post a Comment