Adbox

Monday, September 23, 2019

Akata rufaa kupinga waandishi kusikiliza kesi masheikh Uamsho

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP),  amekata rufaa Mahakama Kuu akipinga wananchi na waandishi wa habari kuingia kusikiliza na kuripoti kesi  ya ugaidi inayomkabili  Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed na mwenzake  22.

DPP amefikia uamuzi huo baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Maira Kasonde kutoa uamuzi akiruhusu waandishi wa habari kuingia katika kesi hiyo wakati unaendelea.

Mahakama iliondoa amri ya kuzuia waandishi wa habari kuandika mwenendo wa kesi hiyo kwa sababu haijafikia katika hatua ya usikilizwaji hivyo ilisema wanaruhusiwa kuiripoti.

Katika rufaa iliyokatwa na DPP wanadai Mahakama ya Kisutu ilikosea kuondoa amri ya Juni 18, mwaka 2015 ya kuzuia wananchi na waandishi kuingia kusikiliza kesi hiyo.

DPP anadai mahakama ilikosea kutoa amri hiyo wakati kuna amri nyingine hivyo asingeweza kutoa tena.

Jamhuri inadai mahakama ilikosea kuamuru wananchi na waandishi kuripoti kesi hiyo wakati kuna zuio.

Katika hoja ya mwisho inadaiwa mahakama ilikosea kuchambua hoja mbalimbali za Jamhuri ambazo zilikuwa zina msingi.

Awali washtakiwa kupitia mawakili wao, Abubakar Salim, Juma Nassoro na wengine waliwasilisha maombi mawili mahakamani ambapo ombi la kwanza walitaka mahakama imshauri DPP kukamilisha upelelezi ndani ya mwezi mmoja na ombi la pili mahakama iondoe amri ya kuwazuia waandishi wa habari kuripoti kesi hiyo.

Mahakama katika uamuzi wake ilimpa njia mbili DPP, moja kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo ndani ya muda mfupi na njia ya pili kama anaona kuna sababu za upelelezi kuchelewa kukamilika aliondoe shauri hilo Mahakamani, akipata ushahidi atawashtaki tena.

“Katika maombi ya kuondoa amri ya  kuripoti  kesi hiyo, mahakama inaondoa amri hiyo, hiyo amri ilitolewa bila kudhamiria kwa sababu kifungu namba 34 cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi kinahusu mamlaka ya Mahakama Kuu, Mahakama Kuu ndio inaweza kutoa amri hiyo kwa sababu sheria inazuia kuandika jina na kutoa picha ya shahidi wakati wa usikilizaji wa kesi .

“Kwa hatua iliyofikia kesi hii, usikilizwaji bado hivyo waandishi wanaruhusiwa kuingia na kuandika kwa lengo la kutenda haki,” alisema.

Kesi hiyo namba 29 ya mwaka 2014 ilifunguliwa mahakamani hapo Agosti mwaka 2014

No comments:

Post a Comment

Adbox