Adbox

Tuesday, July 23, 2019

Waziri Mkuu aagiza fedha za maafa Mwanga kuchunguzwa



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kuchunguza fedha za maafa zilizochangwa na wadau wa maendeleo kusaidia wajasiriamali katika soko la Old Mwanga baada ya kuteketea kwa moto hivi karibuni.

Waziri Mkuu ameagiza kuchunguzwa kiasi cha fedha kilichopatikana na matumizi yake ili kujibu malalamiko ya baadhi ya wajasiriamali na wananchi wanaozunguka soko hilo wanaodai zimefujwa.

Alitoa agizo hilo wakati akizungunza na watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo na baadhi ya wananchi waliokuwa wakilalamikia matumizi ya fedha hizo.

Aliagiza kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kufuja fedha hizo kwani kitendo hicho kinawaondolea wananchi imani katika kuchangia mambo ya maendeleo.

"Baada ya soko kuungua, wadau ikiwamo Benki ya NMB walitoa michango yao hivyo wangependa kufahamu nini kilipatikana na matumizi yake ni yapi, haiwezekani watu watoe fedha zao kisha wasitake kujua zimefanya kazi gani," alisema.

Katika mkutano huo, wananchi walimweleza Waziri Mkuu kwamba soko hilo halina choo cha kudumu baada ya eneo la awali kumegwa na kuuziwa mtu mwingine ambaye amejenga kibanda cha biashara.

Kutokana na malalamiko hayo, Majaliwa alimwagiza Ofisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mwanga kusimamia suala hilo ili kupata taarifa ya jumla ya fedha zilichochangwa.

Kuhusu eneo la choo kujengwa Kibanda, Majaliwa aliagiza kubomolewa ili wananchi wapate huduma zote muhimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Zefrin Lubuva aliahidi kulifanyia kazi suala hilo ndani ya siku nne.

No comments:

Post a Comment

Adbox