Adbox

Wednesday, July 10, 2019

Mahakama za wilaya kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Eliezer Feleshi amesema wamejipanga kuboresha mahakama zote nchini kuanzia ngazi ya wilaya kutumia mfumo wa kielektroniki kwa kuweka taarifa zake zote mtandaoni.

Jaji Kiongozi alitoa kauli hiyo wakati alipotembelea banda la Mahakama katika viwanja vya Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF) yanayoendelea.

Alisema hivi sasa wameanza kusajili kesi kwa mfumo wa kielektroniki na pia majaji na mahakimu wa baadhi ya mahakama wameanza kuweka maamuzi ya kesi mbalimbali mtandaoni ili kurahisisha taarifa. Jaji Feleshi alisema lengo la kufanya hivyo ni kuwapa fursa wananchi kusoma maamuzi ya kesi zote zinazotolewa hukumu kupitia njia ya mtandao badala ya kutumia muda mwingi kusafiri kwenda mahakamani kufuatilia.

"Tumeanza kuboresha huduma za mahakama zetu ili kurahisisha huduma kwa wateja ambao ni wananchi, lakini pia kuokoa muda wao ili wajipange na kufanya kazi nyingine za maendeleo badala ya kufuatilia siku nzima kesi mahakamani,"alisema.

Awali, Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama, Victoria Nongwe alisema hatua hiyo ni mkakati wa kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa mahakama. Akizungumzia mfumo huo, Hakimu Victoria alisema katika mfumo huo mawakili binafsi na wale wa serikali zaidi ya 632 wamepata akaunti tumizi ya kufungua kesi kwa njia hiyo na kwamba tangu kuzinduliwa kwake Februari mwaka huu, mashauri 1,111 yamewasilishwa.

Akifafanua mashauri hayo, Hakumu Victoria alisema kati ya hayo mashauri 365 ya yameshasajiliwa mahakamani, 161 bado yapo kwa mawakili 223 yamerudishwa kwa marekebisho na mengine 66 yamekataliwa.

"Mfumo huu ulianzishwa ikiwa ni mkakati wa mahakama wa kuboresha huduma zake na pia kupunguza malalamiko na kuweka mazingira bora ya utendaji kazi yenye kuepuka uwezekano wa kuwepo kwa vishawishi vya rushwa," alisema.

Alisema hivi sasa wakili aliyepata akaunti tumizi ya kufungua kesi mtandaoni anaweza kufungua kesi akiwa mahali popote, hivyo kurahisisha usajili wa kesi lakini pia iwapo kuna makosa katika usajili huo ombi hurudishwa kwa marekebisho. Kama halikubaliki pia wakili hupata taarifa ndani ya muda mfupi.

No comments:

Post a Comment

Adbox