Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko ameiambia Kamati ya Bunge ya nishati na madini kuwa Kama Wizara wanaendelea na uboreshaji wa masoko ya madini ili yaendane na hadhi ya biashara hiyo tofauti na hivi yalivyo kwa Sasa.
Amebainisha hayo baada ya kamati ya Bunge ya Nishati na madini, kufanya ziara katika soko la madini la Mkoa wa Dodoma na kutoridhishwa na ofisi hizo ambapo wamesema haziendani na hadhi ya bidhaa inayouzwa katika soko hilo na kuitaka Wizara kuboresha ofisi hizo.
Waziri Biteko ameiambia Kamati ya Bunge kuwa serikali ilianzisha masoko hayo ili kudhibiti utoroshaji wa madini uliokuwa umekithiri na kuipotezea Serikali mapato mengi, hivyo wakati wa uanzishwaji wa hawakuzingatia ubora wa ofisi hizo bali walilenga kudhibiti utoroshaji wa madini kwanza ndipo waanze kuboresha ofisi.
"Ndio maana mhe. mwenyekiti leo hatuzungumzii kutokuwepo kwa soko tunazungumzia kuboresha masoko ambayo yapo na umetusaidia Sana, licha ya kuwa hakuna shughuri kubwa Dodoma lakini kiasi tunachokusanya sasa ni Mara nne ya kabla ya soko hili"
"Sio soko la Dodoma tu masoko yote na tumeendelea kuyaimarisha ukienda pale Arusha kwa mfano jengo tuliloanza nalo lilikuwa la ovyo sana halina hata rangi lakini tulilizindua na tukaanza kuliboresha hadi baadaye likawa dogo na tukatafuta eneo lingine" amesema Biteko.
Amesema mwanzo ilikuwa ni watu wajue ni wapi pa kuuzia madini na tunaboresha kadri tunavyokwenda na tulikuwa na soko la Namanga na lilifunguliwa kwa lengo la kuwahi siku ya mwisho ambayo Raisi aliitoa na halikuwa salama na walilifunga na kuendelea kuboresha sehemu nyingine.
Amesema jengo la ofisi ya Madini Mkoa wa Dodoma lipo chini ya Katibu tawala wa Mkoa wa Dodoma hivyo Kama Wizara wataendelea kuwasiliana na katibu tawala ili kuona namna ya kuboresha au kutafuta sehemu nyingine kutokana na ukubwa na hadhi ya Mkoa wa Dodoma.
Amesema serikali imelenga kujenga Ofisi za tume ya madini Dodoma hivyo kama Katibu tawala wa Mkoa wa Dodoma ataona eneo hilo halifai tutashauriana ili kuwa na ofisi nzuri zaidi itakayoenda sambamba na ofisi za tume.
Aidha amesema serikali itakaa ili kuondoa vikwazo na maudhi yanayowakwamisha wawekezaji ili kuwajengea Mazingira mazuri ya biashara amesema hamna haja ya kulalamikia tozo za halmashauri ambazo wateja wao hawazijui ambazo kwenye halmashauri zinatofautiana sana.
"Unaweza kwenda kwenye Halmashauri nyingine wanaipa ushuru wa gari kwamba kila gari inayopita inatozwa elfu kumi unaenda mahala pengine wanatoza kwa tani ,Kuna siku tulifanya ziara Iringa tukakuta tozo zote ukijumulisha unakuta mchimbaji anatozwa asilimia 28, hauwezi kukuza biashara" amesema Waziri Biteko.
Amesema changamoto nyingine ambayo inawakwaza wawekezaji katika sekta ya madini sio serikali ni watu binafsi ambapo mwekezaji ili aonekane mzuri lazima atoe fedha kwa baadhi ya watu ambapo Kama hatoi fedha inaonekana hafai na kuanza kusumbuliwa.
Aidha kamati ya Bunge ya Nishati na madini, pia imetembelea machimbo ya mawe ya nakishi nakishi yaliyopo Ntyuka na Ng'ong'ona unaomilikiwa na kijana wa kitanzania, kuitaka serikali kuendelea kuwasimamia na kuwashauri wawekezaji wazawa ili kufika mbali zaidi katika malengo yao, pia wametembelea ujenzi wa jengo la utawala chuo Cha madini kilichopo Miyuji Dodoma.


No comments:
Post a Comment