Adbox

Thursday, March 5, 2020

Wafamasia watakiwa kudhibiti usalama na ubora wa Dawa

MKURUGENZI wa Idara ya Dawa na vipodozi kutoka wakala wa chakula na dawa Zanzibar Bora Mposanje Lichanda, amewataka wafamasia na wananchi kwa jumla kuhakikisha wanadhibiti usalama na ubora wa dawa kwa matumizi ya binaadamu ili kuepusha kutokea madhara kwa mtumiaji .

Aliyasema hayo  katika ukumbi wa Sanaa wa Rahaleo wakati alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wanaohusika na utafiti wa madhara yanayotokana na dawa  na vipodozi  pamoja na tiba za asili kwa kukumbushana kupeyana mawazo  kujua dawa zinazoleta madhara na usalama wake.

Alisema katika uchunguzi walioufanya wamegundua uwasilishwaji wa matumizi ya  madawa ni mdogo hivyo jukumu la kuhusiana na usalama wa watumiaji wa dawa uwe mkubwa ili uweze kusaidia  changamoto zinazojitokeza.

Amesema katika kudhibiti hili ZFDA inahitaji ushirikiano zaidi na wadau mbali mbali na watu wanaotumia dawa hizo wanaotoa  katika Hospital kwa lengo la kushirikiana nao kwa karibu ili kuhakikisha dawa hizo zinakuwa salama kwa watumiaji na wananchi kwa ujumla.

Aidha amesema takriban  kitaaluma dawa zote huwa na madhara yake iwe ya Hospital au ya miti shamba kwani ukitumia kwa kuzidisha kiwango inaweza kuathiri na pia  dawa hiyo hiyo wengine inatibu na wengine inawaletea madhara kwa kuwatokea ndani ya miili yao na kubadilishiwa na kupewa isiyowathiri.

“Wito wangu kwa jamii iache kula dawa bila kupata ushauri wa daktari ili kujiepusha kutokewa na madhara yanayoweza kujitokeza tumezowea ukijisikia kuumwa na kichwa , au uchovu ndani ya mwili  kula dawa bila ushauri wa daktari tuache mara moja”, alinasihi Mkurugenzi huyo.

Kwa hiyo iwapo itatokea tatizo lolote kwa mtumiaji kutokana na dawa alizotumia ni vyema kwenda katika ile Hospital aliyopewa dawa zile na kutoa ripoti ili kufanyiwa uchunguzi na baadae kupewa tiba nyengine.

Alisema kwa kuwa mkutano huo wa wadau mbali mbali wa kifamasia tuna imani mchanganyiko huo utaleta mashirikiano  mazuri ili kuona ripoti zinawasilishwa na michangio itayotolewa itaweza  kusaidia watu ambao wanaotumia dawa hizo.

Akiwasilisha mada katika mkutano huo mkuu wa usalama na ubora wa dawa kutoka ZFDA  Mohammed Omar Simba   amesema katika utibabu  wa dawa zikitokea kuleta madhara kwa binaadamu itabidi zirikodiwe ili baadae zishughulikiwe  zisiendelee kuleta madhara zaidi na wale waloathirika na dawa hizo wawekwe kwenye rekodi maalum kwa ajili ya ushahidi pindipo utapohitajika.

Kwa upande wake mfamasia wa Hospital ya binafsi kutoka Tawakal Said Rashid alisema kwa upande wa Hospital yao changamoto hizo hazijatokea kwani dawa wanazotumia ni bora na usalama wa hali ya juu.

Vile vile alisema tunaepuka kununuwa dawa ambazo zilizomaliza muda wake ili lisije kutokea tatizo katika utumiaji wa dawa kwa binaadamu na kusababisha madhara.

No comments:

Post a Comment

Adbox