Wakazi wa Kitongoji cha Kwawema, Kijiji cha Kiwangwa halmashauri ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wanauomba uongozi wa (CHALIWASA) sasa DAWASA kuboresha huduma ya maji katika maeneo yao.
Kwanza walianza kuishukuru Serikali kwa juhudi kubwa za kuwapunguzia changamoto ya huduma hiyo, ambapo katika miaka iliyopita hali ilikuwa ngumu ya upatikanaji wa huduma hiyo, hali iliyosababisha kuyatumia maji yasiyosafi na salama.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari kitongojini hapo juzi, wakazi Sauda Juma, Rahma Said, Mussa Farris, Rashid Jombo na Omary Koyo Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, kwa nyakati tofauti walisema kuwa maji bado tatizo.
Sauda na Rahma wakiwa kwenye mtaro uliopo kando ya barabara ya Msata Bagamoyo wakichota maji, walisema kuwa pamoja na kupatikana kwa huduma hiyo mara chache chache tofauti na miaka iliyopita, lakini ameuomba uongozi kuongeza kasi ya upatikanaji wa maji.
"Kama unavyotuona tunachota maji haya yaliyopo katika mtaro, hii inatokana na kutokupatikana maji kwa wakati wenye vituo vilivyojengwa kwa ajili ya huduma hiyo, tunaishukuru Serikali kwa kutupunguzia adha hii ukilinganisha na miaaka iliyopita, tinawaomba waongeze kasi," alisema Sauda.
Nae Rahma alisema kuwa mara ya mwisho kutoka maji kwenye kituo kilicho kwenye eneo lao ni wiki iliyopita, hivyo kulazimika kutumia maji ya katika mtaro, wakati mwingine kwenye kisima cha asili kilichopo eneo la Ndalo.
Jombo msimamizi wa moja ya kituo cha maji katika eneo hilo alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo wananchi wengine wanalazimika kununua maji dumu kwa shilingi 500, bei ambayo ni kubwa kulingana na kipato cha wakazi hao.
Farris alielezea adha wanayoipata wanawake ya kufuata maji kwenye maeneo tofauti, ikiwemo kisima cha asili wneo la Ndalo, huku akiuomba uongozi wa DAWASA kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.
Kwa upande wake Mwenyekiti Koyo aliutaka uongozi RUWASA unaohusika na usambazaji wa maji katika maeneo ya karibu zaidi na wananchi, kufika kwenye kitongoji hicho kwa lengo la kuwaboreshea huduma wakazi wenye uwezo wa kulipia huduma hiyo binafsi.
"Kitongoji changu cha Kwambwera kina wakazi wengi ambao baadhi yao wanajihusisha na kilimo, kutokana na adha ya upatikanaji wa maji imekuwa changamoto kwao ya kuendeleza kilimo" alisema Koyo.



No comments:
Post a Comment