Adbox

Wednesday, February 12, 2020

Waziri Simbachawene na RC Mahenge wawafariji waathirika wa Mafuriko Chipogolo Mpwapwa

Na Enock Magali, Mpwapwa

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, na Mbunge wa jimbo la Kibakwe George Simbachawene na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge wametoa jumla ya kiasi cha Shilingi Milioni nne kwa waathirika wa mafuriko Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma



Hayo yamejiri wakati Waziri Simbachawene alipofanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali katika kata ya Chipogolo yaliyoathiriwa na mvua na kujionea hali halisi ya miundombinu ilivyoathirika pamoja na kuwapa pole wakazi waliopata adha kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.



Akizungumza na wananchi hao Simbachawene amesema kuwa ameguswa na tukio hilo ambapo pamoja na misaada mingine ambapo amekuwa akitoa kupitia viongozi wa kata hiyo kama mbunge wa jimbo hilo anatoa kiasi cha shilingi Milioni moja kwa ajili kuwasaidia wale waliothirika Zaidi na mafuriko.



Aidha pia,amewataka wananchi wa kata hiyo kuacha tabia ya kukata miti hovyo, kujenga nyumba zenye ubora na kutumia mvua zinazoendelea nchini kwa kilimo ili kuwepo chakula cha kutosha.



“Ni kweli mvuahizi zimeleta madhara makubwa sana kwetu,lakini pia tuzitumie kama fursa,kwa huu muda tunaweza kuendelea kupanda mazao na tukavuna ili kufidishia yale yaliyosombwa na maji.usitegemee mpaka uwe na eneo kubwa ndio ulime,tumia eneo lako dogo kulima kilimo chenye tija”Alisema.



“Tujenge maeneo sahihi ili hata vizazi vijavyo vikute , tujenge nyumba bora maana nyingine hata bila mafuriko lazima zitaharibika kama si salama tubadilike kulingana na wakati maana ukikosea sasa utaumia baadae,lakini pia tuache kuharibu mazingira,watu wanakata sana miti na hiyo ndio sababu ya mafuriko haya,tupande miti na tusikate miti milimani”Alisisitiza.



Aidha, ameonyesha kushangazwa na kitendo cha baadhi ya watu wanaobeza kupitia mitandao ya kijamii kuwa licha ya kutokea mafunriko kwenye wilaya hiyo Mbunge haonekani na kuhoji kuwa hata akiwepo atazuia mafuriko kwa mkono.



Pia amewashukuru wananchi hao kwa kuendelea kumuombea na kumuunga mkono na kuwataka kuwapuuza wale wanaojipitisha mitaani na kutoa misaada kwa nia ya kutaka kugombea nafasi ya ubunge katika uchaguzi wa mwezi Octoba mwaka huu.



“Nimesikia kuna watu wanapitapita kwenu kutoa msaada ili baadae waje wagombee nafasi ya ubunge,mimi siwazuii kwa sababu nchi yetu ni ya kidemokrasia,kwa kuwa mpo katika matatizo nyie chukueni misaada yako lakini mnajua wa kumpa kura zenu”Alisema.



Simbachawene amesema ni ukweli usiopingika kuwa mvua ni nyingi na zinaendelea kunyesha nchini lakini haikutakiwa kuwa na madhara makubwa kiasi hicho na kutaka hali hiyo iwe fundisho kwa siku zijazo kwa kujenga nyumba kwenye maeneo yenye miinuko.



Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge yeye amechangia kiasi cha Shilingi Milioni tatu fedha itakayowasaidia waathirika wa mafuriko wilayani humo na kusema kuwa amesema kama mkoa wamekwisha panga na kukubaliana kujenga miundombinu ya uvunaji maji katika kila Wilaya jambo litakalosaidia kupunguza kasi ya maji wakati wa mvua pamoja na maji hayo kutumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo cha umwagiliaji



“Maji ni mengi yamekuwa yakipotea tu bure,sasa kama mkoa tumekwisha kubaliana kujenga miundombinu ya kuyavuna maji hayo,tumekubaliana kujenga mabwawa kwa kila wilaya ili kuyapunguza kasi maji lakini pia maji yatakayovunwa yatasaidia kwenye shuguli za kiuchumi na uzalishaji ikiwemno kilimo cha mbogamboga”Alisema



Naye Mtendaji wa kata Baraka Mahenge akiwasilisha taarifa ya mafuriko ndani ya kata hiyo amesema amesema mafuriko yalianza tangu Novemba 28 mpaka February 07 na mpaka sasa jumla ya nyumba 755 na miundombinu mbalimbali vimeathiriwa.



Katika hatua nyingine Mkuu Wa Wilaya hiyo ya Mpwapwa Jabir Shekhmwer naye alitoa kiasi cha shilingi laki tano na kuahidi kuwapelekea wananchi mahindi yatakayouzwa kwa bei nafuu

No comments:

Post a Comment

Adbox