Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) inaandaa mtaala wa kufundishia kozi ya Diploma ya Sayansi na Teknolojia ya Chakula (Ordinary Diploma in Food Science and Technology) kwa ajili ya kuwapa wahitimu wa kozi hiyo ujuzi wa kuzalisha bidhaa mbalimbali zitokanazo na mazao (value chain addition). Mkuu wa Idara ya Sayansi na Teknolojia ya Maabara, Dkt Florence Mamboya anasema kozi hiyo inatolewa kwenye taasisi na imefikia muda wa kuifanyia maboresho ili iendane na wakati na pia iweze kusaidia wataalamu watakaotoa mchango mkubwa wa kuendeleza sekta ya viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali za vyakula, vinywaji na nyingine zitokanazo na mazao. "Tunafanya mapitio ya mtaala wetu kuifanya kozi hii iwe bora zaidi, wengi wa wahitimu wa kozi hii waende kuzalisha moja kwa moja bidhaa mbalimbali na kujiajiri na pia kutoa ajira kwa vijana wenzao," anasema Dk Mamboya na kuongeza kua mtaala huo utaanza kutumika mwaka ujao wa masomo.
Ameongeza kusema mwanafunzi atakayehitimu kozi hiyo ya diploma anaweza kuajiriwa kwenye viwanda vya vyakula, vinywaji, taasisi za elimu ya juu, pia taasisi za utafiti na pia mashirika kama yalivyokuwa TBS na TFDA.Aidha, anasema uhuishaji wa mtaala huo unakwenda sambamba na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kuchakata bidhaa za chakula kwaajili ya kufundishia na pia kufanya utafiti ili kuleta mapinduzi makubwa ya ubunifu kwenye usindikaji wa vyakula na uongezaji wa mnyonyoro wa thamani kwenye mazao.DIT ilipata ufadhili wa Sh milioni 200 kutoka wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia kwakupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA). Akifungua kikao kazi hicho, Kaimu Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Profesa Patrick Nsimama anasema uboreshaji wa mtaala huo umefanyika kwa kuzingatia dhana ya Taasisi impya ya ufundishaji (Teaching Factory) inayolenga kuwapa wanafunzi ujuzi zaidi.
No comments:
Post a Comment