Adbox

Thursday, February 27, 2020

TANROAD kujenga madaraja korofi Masasi

Na Hamisi Abdulrahmani, Mtwara.

   WAKALA wa barabara mkoa wa Mtwara(TANROAD)imesema kuwa imepanga kutumia kiasi cha sh.511,3 milioni kwa ajili ya matengenezo ya madaraja mawili makubwa ya Mkwaya na Mchauru ambayo yako katika barabara ya Mbuyuni-Makongo’onda wilayani Masasi mkoani hapa.

   Hayo yalisemwa jana mkoani Mtwara na meneja wa TANROAD mkoa wa Mtwara, Mhandisi Doto John wakati wa kikao cha bodi ya barabara mkoa, Mtwara kilichofanyika katika ukumbi wa benki kuu tawi la Mtwara na kuudhuliwa na wajumbe mbalimbali wa bodi hiyo.

   Alisema katika yao ya mwaka wa fedha 20192020 wakala wa barabara mkoa wa Mtwara imepanga kufanya matengenezo makubwa ya madaraja mawili ya Mkwaya-Mchauru ambapo madaraja hayo kwa muda mrefu yamekuwa kero kwa wananchi wa vijiji hivyo.

  Mhandisi John alisema madaraja hayo yapo wilayani Masasi katika kata ya Makong’onda na moja lipo katika kata ya Mchauru katika barabara ya Mbuyuni-Makong’okonda kuelekea wilayani Newala.

   Alisema madaraja hayo yote yatagharimu jumla ya sh.511,3 milioni na kwamba tayari mkandarasi wa kujenga madaraja hayo ameshapatikana ambapo daraja la Mkwaya ujenzi wake umeshaanza kufanyika.

    Alisema madaraja hayo yamekuwa kitovu kikubwa cha uchumi wa wananchi waliozungukwa na madaraja hayo hivyo pindi yatakapokamilika yatafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi.

   “Kwa mwaka huu wa fedha wa 2019/2020 TANROAD mkoa wa Mtwara tumepanga kutumia kiasi cha sh.511.3 milioni kwa ajili ya ujenzi wa madaraja haya mawili tayari daraja la Mkwaya matengenezo yake yameaanza,”alisema Injinia John

   Mhandisi John alisema ujenzi wa daraja la Mchauru utagharimu jumla ya sh.207 milioni huku ujenzi wa daraja la Mkwaya utagharimu sh.304 milioni ambapo yote kwa ujumla yatagharimu jumla ya sh.511.3 milioni.

   Alisema TANROAD itahakikisha fedha hizo zinatumika vizuri na kwa ufanisi zaidi na mkandarasi anafanya kazi ya kiwango cha juu na madaraja hayo na mengine ambayo yatajengwa yanakamilika kwa wakati na yanakuwa yenye ubora mzuri.

  Mhandisi John alisema wakala wa barabara mkoa wa Mtwara wamekuwa wakipita usiku na mchana katika barabara mbalimbali za mkoa wa Mtwara kuwasimamia wakandarasi na kuwapa maelekezo sahihi ya utekelezaji miradi ya wanayotekeleza ya barabara ili miradi hiyo ifanyike kwa ufanisi zaidi.

No comments:

Post a Comment

Adbox