Serikali Mkoani Mtwara, imepiga marufuku vijana mkoani humo kukaa vijiweni bila ya kufanya kazi za kiuchumi badala yake watafute mashamba ya kilimo ili waweze kuongeza tija ya chakula na kipato ndani ya familia.
Agizo hilo limetolewa jana mkoani humo kwa nyakatitofauti na Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa wakati alipokuwa kwenye ziara yake katika wilaya zote za mkoa huo.
Alisema watendaji wa kata,vijji na mitaa mkoani Mtwara wahakikishe hakuna kijana yeyote ambaye anakaa kijiweni bila ya shughuli za kiuchumi.
Byakanwa alisema kijana ambaye atakutwa kijiweni akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo husika vya kisheria ili alipishwe faini ya kukaa bila ya kufanya kazi.
Alisema kila mtendaji kata katika eneo lake ahakikishe anawatambua vijana wote ambao wamekuwa na tabia ya kuamka na kukaa vijiweni kutwa mzima bila kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Byakanwa alisema kumekuwa na kundi kubwa la vijana mkoani Mtwara ambao wamekuwa na tabia ya kukaa vijiweni kuanzia asubuhi mpaka jioni bila kuzalisha chochote jambo linapaswa lisipewe kipaumbele.
"Watendaji wa kata na vijiji mkimkuta kijana yeyote ambaye amekaa kijiweni muda wa kazi mkamateni na mtafutieni shamba akalime na akikataa mfikisheni katika vyombo vya sheria," alisema Byakanwa
Alisema haiwezekani mkoa unakuwa na vijana wengi alafu wamekuwa hawazalishi kwa ajili ya kujipatia kipato ndani ya familia zao na taifa kwa ujumla.
Alisema serikali mkoani humo inahitaji kuwa na vijana ambao ni wazalishaji mali kwa vile Mtwara ni miongoni mwa mikoa yenye eneo kubwa la kilimo hivyo kama vijana wakiamua kulima wataweza kunufaika.
Byakanwa alisema vijana ni nguvu kazi ya taifa hivyo kama wakiwa hawafanyi kazi za kuzalisha hata taifa linaweza kukosa tija katika uzalishaji mali.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Masasi,Selemani Mzee alisema atahakikisha vijana kwenye wilaya yake wanahamasishwa kupenda kilimo ili waweze kujikita na kilimo.


No comments:
Post a Comment