Adbox

Wednesday, January 1, 2020

TRA yavunja rekodi Makusanyo ya Desemba

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk Edwin Mhede amesema wamefanikiwa kukusanya Sh4.972 trilioni kati ya Sh5.1 trilioni walizopanga kukusanya katika kipindi cha robo ya pili inayohusisha Oktoba, Novemba na Desemba, 2019.

Dk Mhede ameeleza hayo leo Januari Mosi, 2020 wakati akitoa ripoti kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya TRA Dar es Salaam.

Amesema makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 19.78 ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha robo ya pili cha mwaka 2018/19 ambapo mamlaka hiyo ilikusanya Sh4.151 trilioni sawa na ufanisi wa asilimia 87.59, wakati lengo lilikuwa kukusanya Sh4.739trilioni.

" Makusanyo haya ni mwendelezo wa kiashiria cha wazi kwamba walipakodi na wananchi walio wengi wana uelewa na kukubali kulipa kodi. Rai yangu asiwapo mlipakodi hata mmoja ambaye atathubutu kubaki nyuma," amesema Dk Mhede.

Akizungumzia takwimu za kila mwezi, Dk Mhede amesema Oktoba walikusanya Sh1.484 trilioni, Novemba Sh1.501 trilioni na Desemba Sh1.987 trilioni akisema ni mwezi uliovunja rekodi.

No comments:

Post a Comment

Adbox