Hali hiyo imetia hofu wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa Kigoma, ambao wameeleza kutishwa na kasi kubwa ya kuzaliana kwa wakimbizi hao. Hivyo, wameitaka serikali kuchukua hatua kukabiliana na hali hiyo.
Wajumbe hao walitoa kauli hiyo kwenye kikao cha siku moja cha kawaida cha halmashauri hiyo. Walisema kuwa kuendelea kuzaliana holela kwa wakimbizi hao, kutakuwa na madhara makubwa siku zijazo kwa nchi, ikiwemo baadhi ya wakimbizi hao kudai taifa lao ndani ya Tanzania.
Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko alisema ametembelea baadhi ya kambi za wakimbizi mkoani Kigoma na takwimu ya watoto 600 wanaozaliwa kila mwezi kwenye makambi hayo ni kubwa sana. Nsanzugwanko alisema kama kambi moja, inaweza kuwa na watoto 600 wanaozaliwa, inakuwaje ukijumlisha kambi zote na kwa mwaka mmoja.
Alisema idadi hiyo ni kubwa na isipowekwa mkakati sasa hivi, athari za baadaye ni kubwa.
Alitaja athari ya baadaye ni sehemu kubwa ya watoto hao waliozaliwa, kujichanganya mtaani na kuishi kama raia wengine, ambayo italeta hatari ya usalama wa nchi.
Katika mapendekezo yake, alisema kuwa ni vizuri serikali ichukue jukumu la kuhakikisha wakimbizi hao, wanarudishwa kwao haraka au wanapewa uraia kwa masharti maalum, ili uwezekano wa kuzuka mambo yasiyo kwenye taratibu, usiweze kutokea.
Katibu wa CCM wilaya ya Kibondo, Stanley Mkandawile alisema ongezeko kubwa la wakimbizi na idadi kubwa ya wakimbizi wanaotoroka kambini na kuishi mtaani, linaongeza matatizo ya utata wa uraia wa wananchi wa mkoa Kigoma ikiwemo nyakati za uchaguzi, jambo ambalo linaweza kuwafanya baadhi ya wakimbizi kupata nafasi za uongozi.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Kirumbe Ng’enda alilalamikia ongezeko hilo kubwa la kuzaliana kwa wakimbizi.
Pia, alilalamikia manyanyaso wanayopata wananchi wa mkoa Kigoma, kuhusu utata wa uraia na kuwafanya wananchi wa mkoa huo kuwa raia wa daraja la tatu.
Katika kuondoa hilo, Ng’enda aliunga mkono kurudishwa kwao wakimbizi wote wanaoishi kwenye makambi mbalimbali mkoani Kigoma, sambamba na serikali kuhakiki uraia wa wananchi wa mkoa huo.
Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma, Amandus Nzamba alisema azimio la wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa Kigoma, ni kuitaka serikali kuangalia upya suala la kushughulikia utata wa uraia wa wananchi wa mkoa huo, sambamba na kuangalia ongezeko kubwa la kuzaliana kwa wakimbizi hao.
No comments:
Post a Comment