Kwa upande wa chama tawala, wapo waliojichanganya kwa kushindwa kutumia vizuri ‘nyama ya ulimi,’ wakazungumza bila breki, lakini baadaye, wakatambua kosa lao; wakajitambua kuwa ni wana wapotevu; wakarudi nyumbani kwa baba na kuomba radhi. Uchungu wa mwana ajuaye mzazi; Rais John Magufuli akawasamehe. Hao, ni January Mamba, Nape Nnauye na William Ngeleja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa upande wa upinzani, uwajibikaji ukapungua kwa baadhi ya wabunge; wakashindwa kufanya kazi kwa mfumo rasmi na badala yake, wakataka kufanya kwa mazoea, bila kujali kwamba zama za kutenda kwa mazoea zimekwisha. Hao wakajikuta wanajivua ubunge bila kujua. Hao ni Joshua Nassari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
MAGUFULI ANAWASAMEHE WABUNGE WALIOMSEMA VIBAYA
Mwaka ulioisha wa 2019 umekuwa na mambo mengi ambapo kati ya mambo hayo ni pamoja na kuvuja kwa sauti za wanasiasa vijana wabunge wa CCM zilizoaminika kuwa ni za Nape (Mbunge wa Mtama), January Makamba (Mbunge wa Bumbuli) na William Ngeleja (Mbunge wa Sengerema). Sauti za wanasiasa hao wa CCM zikasikika zikitoa maneno ya kumkejeli Rais John Magufuli ambaye pia licha ya kuwa ni rais wa nchi, pia Mwenyekiti wa chama chao (CCM).
Sauti hizo zilisambaa katika mitandao ya kijamii. Hata hivyo, Septemba 4,2019 wakati Rais Magufuli akahutubia katika mkutano wa wataalamu wa ujenzi nchini, alisema wabunge Makamba na Ngeleja walimuomba msamaha na kuwa amewasamehe.
Akasisitiza: “Kuna umuhimu wa kusameheana hasa mtu anapokukosea na mimi nimewasamehe.” Rais ambaye ni mwenyekiti wa kitaifa wa CCM akasema: ‘Nilizisikia zile sauti na nikasema kuwa hivi hawa wakipelekwa kwenye Kamati ya Maadili ya CCM adhabu si itakuwa kubwa, lakini wawili walijitokeza na kuniomba msamaha ambao ni Makamba na Ngeleja, nimewasamehe.”
Kwa kurejewa na busara kama walivyofanya wenzake, siku kadhaa baadaye, Nnape naye aliwasili Ikulu –Magogoni na kumuomba radhi Rais Magufuli na kisha wote wamesamehewa na kuendelea na kazi zao kama kawaida katika majimbo.
WABUNGE WA CHADEMA ‘WAJIPOTEZEA’ UBUNGE
Aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, ‘anakitia kitumbua mchanga’; anapoteza ubunge wake. Kivipi? Machi 14, 2019, Spika wa Bunge, Job Ndugai alimwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage kumjulisha kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki lililokuwa likiongozwa na Nassari lipo wazi kutokana na mbunge huyo kupoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge.
Ndugai akasema Nassari amekosa sifa za kuendelea na ubunge wake kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu ya bunge ambayo ni Mkutano wa 12 wa Septemba 4- 14, 2018, Mkutano wa 13 wa Novemba 6- 16 2018 na Mkutano wa 14 wa Januari 29 mpaka Februari 9, 2019.
Kwamba uamuzi wa spika umezingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71(1)(c). Ibara hiyo inasema: “Mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake cha ubunge ikiwa ataacha kuhudhuria vikao vya mikutano ya bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya spika.”
Ibara hiyo tena imefafanuliwa pia katika kanuni ya 146(1) na (2) za kanuni za kamati ya kudumu za bunge toleo la Januari 2016. Kanuni hiyo inaeleza: “Kuhudhuria vikao vya bunge na kamati zake ni wajibu wa mbunge, mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano ya bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya spika iliyotolewa kwa maandishi atapoteza ubunge wake na spika ataitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi.”
Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ‘ilibariki’ kuvuliwa ubunge kwa Nassari. Jaji wa mahakama hiyo, Latifa Mansour alikubaliana na uamuzi wa Spika kuwa Nassari amepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na utoro.
Katika utetezi wake kabla ya kwenda mahakamani, Nassari alidai kuwa alikuwa nje ya nchi akimuuguza mkewe na kuwa, aliwasiliana na Ofisi ya Spika kwa kuongea kwa simu na msaidizi wake pamoja na kutuma ujumbe kupitia barua pepe. Baada ya wanachama wa vyama vingine kushindwa kukidhi vigezo, mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo, Dk John Pallangyo alipita bila kupingwa na akaapishwa Mei 22, 2019 bungeni jijini Dodoma.
Tundu Lissu wa Singida Mashariki Sikio la kufa halisikii dawa. Ingawa wahenga walisema mwenzio akinyolewa, wewe tia maji, Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki, hakujifunza kwa Nassari.
Ndiyo maana Juni 28, 2019, Spika Ndugai akatangaza kumvua ubunge Lissu. Alitoa sababu mbili kubwa kuwa ni pamoja na Lissu kutotoa taarifa rasmi ya maendeleo yake huku akionekana ‘huku na kule’ pamoja na kutokujaza fomu za maadili ya viongozi za Tume ya Maadili, hivyo kupoteza sifa za kuwa mbunge. Ndugai akaliambia Bunge: “Nimemwandikia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kuwa Kiti cha Ubunge wa Singida Mashariki ambacho Mbunge wake ni Tundu Lissu, kipo wazi.” Nafasi ya Lissu katika jimbo hilo imeshikwa na Miraji Mtaturu aliyeapishwa Septemba 3, 2019 bungeni, Dodoma.
WABUNGE WALIOPATA UWAZIRI
Mwaka 2019 ulikuwa mwaka mzuri kwa baadhi ya wabunge baada ya kuuteuliwa na Rais kuingia katika kada ya uwaziri akiwamo Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene aliyeteuliwa Julai 21, mwaka jana kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Muungano na Mazingira), badala ya January Makamba ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Simbachawene anarejea kwenye baraza la mawaziri baada ya kujiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini Septemba 2017. Mwingine ni Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe aliyeteuliwa na Rais Magufuli kushika wadhifa wa Naibu Waziri wa Kilimo. Nafasi hiyo ilikuwa ikikaliwa na Innocent Bashungwa aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Makala haya yameandaliwa na Evance Ng’ingo na Tuzo Mapunda.
No comments:
Post a Comment