| Picha ya Maktaba |
Imeelezwa kuwa chanzo cha ndoa za utotoni katika Mkoa wa Shinyanga ni wazazi na walezi kufanya maelewano wakiwa katika vilabu vya pombe wakinunuliana ili kufikia makubaliano.
Wakizungumza katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto yaliyoandaliwa na shirika la World Vision wananchi wa kijiji cha Penzi katika halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga wamesema mara nyingi ndoa za utotoni katika kijiji hicho hufanyika katika vilabu vya pombe.
Mmoja wa wananchi hao Baruhya Masanja amesema maelewano hayo hufanywa baina ya wazazi au walezi wa pande zaote mbili kwa upande wa mwanaume pamoja na msichana na baada ya hapo zoezi linalofuata ni mtoto wa kike kulazimishwa na wazazi wake kuolewa bila ridhaa yake.
Amesema mipango ya ndoa husika hufanyika nje na mazingira ya nyumbani na siku ya harusi muolewaji hufichwa na kuwekwa ambaye sio sahihi hivyo wanaiomba serikali kuendelea kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwani vijijini hali kama hiyo hawajui kama ni ukatili wa kijinsia kwa kumnyima mtoto haki yake ya msingi ya maamuzi.
Kwa upande wake askari wa jeshi la polisi dawati la jinsia Mkoa wa Shinyanga Brightone John amesema wananchi na wakazi wa eneo husika watambue kuwa hata akiwa sio mtoto wake ana haki ya kumtetea na kutoa taarifa katika jeshi hilo.
Amesema wananchi wamekuwa waoga kutoa taarifa kwa jeshi la polisi kitu ambacho wanajinyima haki yao ya msingi hivyo jeshi hilo lipo kwa ajili ya kusimamia sheria za nchi na endapo mtu asipotoa taarifa na kubainika kuwa miongoni mwa walioshiriki nae atachukuliwa hatua.
Amesema wazazi na walezi wahakikishe hawakubali kudanganywa na watu wasio wema kwa watoto wao kuwapeleka mjini kufanya kazi za ndani na kuwakatisha masomo na akitokea mtu wa namna hiyo watoe taarifa ili sheria ifuate mkondo wake.
Aidha siku ya kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia duniani inatarajiwa kufanyika Disemba 10 mwaka huu ikiwa na kaulimbiu isemayo “kizazi chenye usawa simama dhidi ya ubakaji”


No comments:
Post a Comment