Adbox

Monday, December 30, 2019

UWT watakiwa kuweka ushirikiano katika kuimarisha Chama

Na Thabit Madai-Zanzibar

Mwakilishi wa Jimbo la Chumbuni Miraji Khamis Kwanza  amewataka kina mama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Wilaya ya Amani kuweka mashirikiano katika kukimarisha chama ili kiweze kupata ushindi ifikapo 2020.

Hayo ameyasema huko katika Ukumbi wa Tawi la CCM Kilimani  wakati alipokuwa akifungua  kikao cha  Baraza la UWT Wilaya ya Amani  na kuwataka kuzidisha mashirikiano kwa lengo la kukiimarisha Chama cha Mapinduzi.

Amesema hivi sasa wakati wa Daftari la kudumu umeshafika hivyo kina mama wasimame katika kuhamasisha kwenda kujiorodhesha  na pia kuwahimiza vijana waliofikia umri wa miaka 18 kwenda kujiandikisha ili waweze kupiga kura.

Aidha alisema Daftari linahitaji kuimarishwa kuhamasishwa  na kutiwa hamasa ambapo kina mama wa UWT ndio Viongozi  wasimamizi wa mambo  mbalimbali ya maendeleo.

"Daftari limeshafika tuitumie fursa kwa kujiandikisha kwa kila mwenye sifa na vijana wetu tuwahimize kwa kila aliyefikia umri", alisema Mwakilishi huyo.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Amani,  Fatma  Hamrani amewataka kina mama kuliongoza gurudumu  la maendeleo hadi kulifikisha ukingoni kwa salama na kupiga kura kwa amani na kudumisha mashirikiyano yaliyokuwepo.

Nae Katibu wa UWT Wilaya ya Amani Asha Mzee Omar akisoma taarifa ya utendaji wa kazi za UWT kwa Kipindi cha January hadi Decemba 2019  alisema uhai wa chama ndani ya Wilaya hiyo imezidi kuimarika zaidi kwa kuongeza wanachama wapya 1,454 ambapo zamani walikuwa 3,573 na kuweza kufikia 5,027.

No comments:

Post a Comment

Adbox