Adbox

Wednesday, November 20, 2019

Kiwango cha udumavu kwa Watoto chapungua nchini

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameongoza Mkutano wa 20 wa Kisera wa Wadau wa Sekta ya Afya uliofanyika jana Jijini Dodoma.

Katika Mkutano huo Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wadau imefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi mapya ya VVU kwa Asilimia 20 kwa watu wazima na Asilimia 31.3 kwa Watoto walio chini ya umri wa miaka 15 katika mwaka 2010 hadi 2018.

Aliendelea kusema kuwa, Tanzania imeweza kuongeza kiwango cha upimaji Malaria kutoka Asilimia 64 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 99mwaka 2018, na kufanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa Asilimia 63 kutoka watu 6,737 hadi vifo 2,540.

Aidha, Waziri Ummy amedai kuwa, kiwango cha udumavu kwa Watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kimepungua kutoka Asilimia 34.4mwaka 2015 mpaka 31.8 mwaka 2018.

Katika kikao hicho, Wadau wamekubaliana kutekeleza maeneo ya vipaumbele vilivyopitishwa, ikiwemo, kuboresha utekelezaji wa mikakati ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto, kuboresha utoaji wa huduma za uzazi kwa vijana wadogo, kuboresha utoaji wa huduma za dharura na kushirikiana na wadau kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi wa Afya.

No comments:

Post a Comment

Adbox