Adbox

Saturday, October 19, 2019

Waziri Prof. Ndalichako atoa siku 14 kwa Kamishna wa Elimu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ametoa siku 14 kwa Kamishna wa Elimu kuhakikisha anawasilisha mapendekezo ya namna ya kurekebisha waraka wa elimu unaoruhusu mwanafunzi awe mtoro bila kutoa taarifa ndani ya siku tisini.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari Bogwe iliyoko Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma ambapo amesema waraka huo hauko sawa na wanafunzi wanautumia vibaya kwa kutokwenda shule jambo linalowapelekea kukosa masomo.

Amesema ni lazima sasa kuwa na mfumo ambao mwanafunzi anapokuwa haonekani shuleni ndani ya muda ambao wataalamu wataona ni muafaka mzazi apate taarifa kwani taratibu zilizopo sasa ni za kuwadekeza wanafunzi.

” Kama mwalimu asipofika shule ndani ya siku tano amejifukuzisha kazi, iweje mwanafunzi siku tisini?uwiano uko wapi? Kamishna hili jambo nimeshalizungumza na umeanza kulifanyia kazi tangu mwezi wa saba. Muda ni mrefu nilizungumza katika kikao cha Wizara. Kamilisha kazi na watendaji acheni uzito, angalia kazi ya Mhe. Rais na mimi Waziri wenu, twende pamoja vinginevyo utakaa pembeni,” aliongeza Waziri Ndalichako.

Katika hatua nyingine, Waziri Ndalichako amewataka wanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Bogwe kusoma kwa bidii ili kufuta historia ya matokeo mabaya ya mitihani ya Taifa katika shule hiyo kwani Serikali imetumia fedha nyingi kuwekeza kwenye miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule nchini ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira mazuri.

“Ukiangalia kwa mfano katika shule yenu hii ya Bogwe Serikali imetoa shilingi milioni 378 ambazo zimejenga miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukumbi ambao mnafanyia mahafali sasa kazi iliyobaki kwenu ni nini? someni kwa bidii hamna cha kulaumu Serikali imetelekeza kazi kwenu sasa,” aliongeza Waziri Ndalichako.

Amewataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri na mfano mzuri wa kuigwa mahali popote watakapokuwa ili kuijengea sifa shule waliyosoma na kuwa wazalendo na Taifa ikiwa ni pamoja na kuilinda nchi kwa gharama yoyote.

No comments:

Post a Comment

Adbox