Adbox

Saturday, October 26, 2019

Watoto 1000 wanaozaliwa nchini, watatu huzaliwa na ulemavu wa kichwa kikubwa

Watoto 1000 wanaozaliwa kila siku nchini watatu wanazaliwa wakiwa na matatizo ya ulemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi idadi ambayo imeelezwa kwa mwaka inafikia watoto 4800.

Takwimu hizo zilitolewa leo na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akizungumza katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kichwa kikubwa na mgongo wazi duniani.

Maadhimisho hayo yalifanyika Kitaifa kwenye viwanja wa Tangamano mjini Tanga ambapo alisema kwamba serikali imekuwa ikiweka juhudi kubwa kuweza kuhakikisha inatokomeza suala hilo.

Alisema kwamba wakati umefika jamii kuacha kuwa na mila potofu kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi na dhana hiyo ianze kwa wazazi, walezi na familia inayowazunguka.
“Kwani imani potufu ndio zimepelekea wazazi na walezi wa watoto hao kutumia fedha nyingi kwa waganga wa kienyeji bila mafaanikio na kusababisha ongezeko la vifo vya watoto wao”Alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy aliitaka jamii kutambua kwamba mtoto akizaliwa na kichwa kikubwa sio laana,mkosi wala balaa huku akiwataka kuachana na imani potufu kwani wameambiwa na wataalamu chanzo cha watoto kuzaliwa hivyo ni kutokana na upungufu wa madini ya foliki Acidi na virutubisho muhimu vinavyotokana na kwenye vyakula nyingi vilivyopo hapa nchini.

“Lakini pia niwaase wakina mama wajawaziti kutumia vitamin hiyo kabla ya kupata ujazito huku akitoa wito kwa wanawake wenye umri wa kuzaa miaka 15 hadi 49 kuzingatia ulaji bora wa vyakula vyenye vitamin ya aina ya foliki acidi ikiwemo mbogamboga na matunda,”alisema Waziri Ummy.

Hata hivyo alisisitiza umuhimu wa kila mwanamke aliyefikia umri wa kuzaa wajawazito kwenda kliniki mapema mara wanapogundua ni wajawazito ili waweze kupatiwa huduma za afya ikiwemo vidonge vyenye vitamini ya foliki acid.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella alisema kwamba tatizo hilo linazuilika na kumalizika kabisa kwenye jamii kwa kutoa elimu namna ya kuepukana nalo.

No comments:

Post a Comment

Adbox