Adbox

Saturday, October 26, 2019

Changamoto ya umeme yaitesa shule, Walimu wawapigia goti wazazi

Na Amiri kilagalila-Njombe

Shule ya Sekondari Mount Kipengele iliyopo wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe inakabiliwa  na changamoto ya umeme kwa zaidi ya miezi mitano kutokana na kuungua kwa transfoma iliyopo karibu na shule hiyo.

Kutokana na hali hiyo takribani majengo ya kidato cha tano na cha sita yenye madarasa nane,baadhi ya madarasa na nyumba za walimu ndizo zinazopata umeme kwa kiasi kidogo kupitia kituo hicho kilichopatwa na shida,huku majengo mengine yakiwa na kiza,hatua inayoilazimu bodi ya shule kwa kushirikiana na wazazi kuanza kutafuta panel za solar kwa ajili ya maandalizi ya wanafunzi wa kidato cha nne wanaotegemea kuanza mtihani wao hivi karibuni.

Aidha mkuu wa shule hiyo Mwl Belnow Boniface Mhanga hii leo mara baada ya mahafali ya kidato cha nne yaliyofanyika shuleni hapo,ameeleza kuwa shirika la umeme Tanzania Tanesco wilaya ya Wanging’ombe limeahidi kuitatua changamoto hiyo kupitia gridi ya taifa kuanzia mwezi Novemba.

“Kwa sasa imechukua takribani miezi mitano,majengo takribani nane ya kidato cha tano na sita,lakini na baadhi ya nyumba za waalimu yanapata umeme huu ambao unatokana na umeme huu ambao transfoma iliyoungua nayo imebakiza njia moja, kwa hiyo maeneo mengine kama ya mabweni na madarasa  kidogo kumekuwa na changamoto ambayo hadi sasa tunasubiri Tanesco watuletee umeme,lakini wakati tunasubili basi shule na bodi yake imeamua inunue panel za solar zifungwe kwanza kwenye madarasa ili kutoa nafasi kubwa kwa watoto kujiandaa tunapoelekea kwenye mitihani hii ya taifa”alisema Belnow Mhanga mkuu wa shule

Debora Masimba na Muksin Kaunya ni baadhi ya wanafunzi katika  shule hiyo,wanasema tatizo la umeme limekuwa ni changamoto kubwa kwa wanafunzi hususani wanapohitaji kujisomea.

Baadhi ya wazazi wenye watoto shuleni hapo akiwemo Jordan Mtewele,wamesema uongozi wa shule umeendelea kushirikiana na wazazi ili kuona njia bora ya kutatua changamoto hiyo huku wakisubiri shirika la umeme Tanzania Tanesco wilaya ya Wanging’ombe kutatua changamoto hiyo.

Yusuph Yahya ni afisa taaluma wilaya ya Wanging’ombe,ameshirikiana na wazazi pamoja na waalimu wa shule hiyo, kuchangisha shilingi laki tatu na elfu sabini tano katika mahafali ya 13 ya kidato cha nne itakayoweza kuanza kununua panel za solar.

Kwa upande wake meneja wa Tanesco wilaya ya Wanging’ombe Francis Mvukiye amesema anatambua changamoto hiyo hivyo wamekwisha ombea mradi na tayari tatizo hilo linashughulikiwa.

“Ni kweli kuna changamoto katika ile sekondari na nimeshaombea mradi,na ukawa umepitishwa,lakini katika miradi mikubwa ya Wanging’ombe inayotakiwa ifanyike kwa haraka zaidi ilikuwa ni miradi mitatu,ambayo ni Kipengere sekondari,Igosi na kwa mheshimiwa Philip Mangula, kwa hiyo kazi imeanza kwa Philip Mangula na wakimaliza wanaanza kupeleka umeme Kipengere Sekondari,”alisema Mvukiye.

No comments:

Post a Comment

Adbox