Adbox

Sunday, October 20, 2019

Wanafunzi wavishwa maboxi wakifanya mtihani kukabiliana na udanganyifu

Maafisa katika shule moja nchini India wameomba msamaha baada ya picha ya kushangaza ya wanafunzi waliovalia maboxi vichwani mwao wakifanya mtihani kusambaa katika mitandao ya kijamii.

Picha hizo zilipigwa wakati wa mtihani wa kemia katika shule ya upili ya Bhagat mjini Haveri, jimbo la Karnataka.

Ziliwaonesha wanafunzi wakiwa wamevalia maboxi yaliokatwa upande mmoja, ili kuwazuia wasiibie kazi ya wenzao.

Msimamizi wa shule hiyo ameomba radhi kwa maafisa wa wilaya wa elemu kufuatia kisa hicho.

MB Satish aliiambia BBC kuwa waliamua kutumia mbinu hiyo isiokuwa ya kawaida kukabiliana na visa vya udanganyifu wakati wa mtihani.


Alisema kuwa shule hiyo ilichukua hatua hiyo kama ''sehemu ya majaribio'' baada ya kusikia inatumika katika maeneo mengine nchini.

Pia alisistiza kuwa wanafunzi wenyewe waliridhia kuvalia maboxi hayo vichwani wakati wa mtihani na kuongeza kuwa walikuja nazo wenyewe.

"Hakuna mwanafunzi aliyelazimishwa kuvalia boxi kichwani. Kama unavyoona katika picha hizi kuna baadhi ya wanafunzi ambao hawajazivalia," alisema. "Waliokuwa wamevalia pia baadhi yao walivua baada ya dakika 15, wengine baada ya dakika 20 na hata sisi wenyewe tuliwwambia wazivue baada ya saa moja."

Maafisa wa elimu wa kikanda waliripotiwa kufika shuleni hapo kulalamikia hatua hiyo muda mfupi baada ya picha hizo kusambazwa katika mitandao ya kijamii.

SC Peerjade, naibu mkurugenzi wa wa bodi ya usimamizi ya shule hiyo alitaja hatua hiyo kuwa ya "kidhalimu".

"Nilipopata ujumbe kuhusu kisa hicho, nilitoa agizo kwa usimamizi wa shule kusitisha mpango huo mara moja," alinukuliwa na na gazeti la Time nchini India akisema.

Wakuu wa shule wamesema wamekomesha zoezi hilo kufuatia maagizo kutoka kwa bodi ya shule.

No comments:

Post a Comment

Adbox