Adbox

Saturday, October 26, 2019

Walimu kumi wa shule za msingi na sekondari Kilwa wafikishwa Mahakamani

Na Ahmad Mmow, Lindi

Walimu kumi wa shule za msingi na sekondari wilayani Kilwa, mkoani Lindi wameshitakiwa mahakamani kwa tuhuma za kujihusisha kimapenzi na wanafunzi.

Jana, akizungumza na Muungwana Blog baada ya kumalizika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Lindi, mkuu wa wilaya hiyo Christopher Ngubiagai alisema tatizo la mimba za utotoni katika wilaya hiyo ni kubwa.

Ngubiagai alisema katika kukabiliana na tatizo hilo watu kadhaa wakiwamo walimu kumi wa shule za msingi na sekendari wamefikisha mahakamani kwa tuhuma za kufanya mapenzi na wanafunzi wao. Alisema hali hiyo inadhihirisha ni kwakiasi gani baadhi wa watumishi wa umma ambao wanadhamana ya kuwalinda watoto wanavyochingia kukatiza ndoto za watoto hao. Badala yake wamekuwa ni miongoni mwa wanaosababisha tatizo hilo.

Hata hivyo Ngubiagai kwa masikitiko makubwa aliwalaumu baadhi wazazi na walezi wilayani humo kuchangia kuchelewesha kesi kutolewa uamuzi.

''Japokuwa waliofikishwa mahakamani ni wengi lakini hadi kufikia tarehe 10.10.2019 nikesi nne tu zimetolewa uamuzi,'' alisema Ngubiagai.

Mkuu huyo wa wilaya alibainisha kwamba kinachochangia mashauri hayo kuchelewa kutolewa uamuzi ni wazazi na walezi kutokwenda mahakamani au kutoa ushahidi dhaifu dhidi ya washitakiwa.

''Wanahurumiana na kuoneana aibu. Wanapokwenda polisi wanatoa ushirikiano kwasababu ya woga, lakini wakitoka na kurudi nyumbani wanafundishana jinsi ya kuwalinda wahalifu, ndipo wanapotoa ushahidi dhaifu,'' alisema kwa masikitiko.

Ngubiagai aliyejiapiza kuendeleza mapambano dhidi ya  wanaofanya vitendo hivyo alitaja sababu nyingine inayochangia mimba za utotoni ni baadhi ya madereva wa malori na wasaidizi wao kuwalaghai wanafunzi wanaoishi mbali na shule kwakuwasaidia usafiri( lifti), ndipo huwalaghai na kufanyanao mapenzi.

 Aliweka wazi kwamba waathirika wa lifti za malori ni wanaosoma kwenye shule zilizopo pembeni mwa barabara kuu ya Dar-es-Salaam- Lindi, Mtwara hadi Songea. Hasa kwenye vituo ambavyo malori husimama na kulazwa baada ya usiku kuingia.

 Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni Somanga, Nangurukuru, Kiranjeranje na Hotelitatu ¥ Alitoa wito kwa wazazi na walezi washiriki  mapambano hayo.

Badala ya kuendelea kulindana na kuamini kwamba jukumu na wajibu kukomesha vitendo hivyo ni waserikali peke yake.

 Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika ofisi za idara ya elimu ya mkoa wa Lindi, wilaya ya Kilwa inaongoza kwa wanafunzi kutiwa mimba. Ikielezwa kwamba katika kipindi cha kuanzia Januari hadi hadi mwezi huu( Oktoba) ilikuwa na jumla ya wanafunzi 52 walitiwa mimba na kukatizwa ndoto zao katika maisha yao ya baadae.

No comments:

Post a Comment

Adbox