Adbox

Friday, October 25, 2019

Tsh. Bilioni 10.7 kujenga Chuo cha VETA wilayani Chato

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga jumla ya Shilingi bilioni 10.7 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa chuo hicho, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema ujenzi wa chuo huo unatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.

"Nawapongeza viongozi wa Halmashauri ya Chato kwa usimamizi mzuri kwani mpaka sasa mradi huu umefikia asilimia 78 huku mkandarasi akiwa ameshalipwa asilimia 41 ya pesa yote jambo linaloonyesha kwamba kuna fedha itabaki ambayo itasaidia kuongeza majengo mengine," amesema Waziri Ndalichako.

Aidha, Waziri Ndalichako amewataka Wakandarasi na Washauri Elekezi wanaofanya kazi za Wizara ya Elimu kuwa wazalendo na kuacha kuongeza gharama za miradi inayotekelezwa na wizara hiyo.

"Tumegundua katika mikataba mingi malipo ya washauri elekezi yanalipwa kulingana na kiwango anacholipwa mkandarasi hivyo kufanya mkandarasi kuongeza gharama na kutokukagua vizuri miradi hiyo," ameelezea Profesa Ndalichako.

Waziri huyo amesema Wizara inafanya mapitio hata kwa miradi iliyoishakamilika ili kujiridhisha na gharama halisi za utekelezaji na kuwezesha kutoa fedha zinazolingana na gharama na kuhakikisha miradi inakamika kwa viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema ujenzi wa chuo hicho cha kipekee mkoani humo ni mwendelezo wa mageuzi makubwa yanayoshuhudiwa katika sekta ya elimu kwa kipindi cha uongozi wa serikali ya Awamu ya Tano.

"Chuo cha VETA Chato kitakuwa cha kwanza chenye ubora wa juu katika kanda ya ziwa kwa kuwa ni kikubwa na kitakuwa na karakana zenye vifaa vya kisasa ambavyo vitawezesha vijana wa Chato kuwa na ujuzi na maarifa," amesisitiza Mhandisi Gabriel.

Aidha, Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani ameishukuru serikaki kwa kujenga chuo hicho na kuahidi kuhakikisha anahamasisha vijana wa Chato kujiunga katika chuo hicho ili kupata ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi kupitia viwanda.

No comments:

Post a Comment

Adbox