Adbox

Monday, October 21, 2019

TAMSA yatakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili

Na Thabit Madai,Zanzibar.

Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed ameitaka Jumuiya ya Madaktari Wanafunzi Tanzania {TAMSA) kufanya kazi  kwa kufuata maadili ili kuepuka kwenda kinyume na utaratibu wa udaktari.

Hayo aliyasema huko katika Uwanja wa Mapinduzi Square wakati alipofunga zoezi la huduma ya afya kwa wananchi wa Zanzibar lililoandaliwa na  Jumuiya ya Madaktari Wanafunzi Tanzania.

Alisema suala la maadili ya kazi hasa kwa wale madaktari wanafunzi hupaswa kuzingatia kutokana na kanuni za kazi  kwani kuepuka maadili kunateremsha hadhi ya udaktari.

“Kuitumia lugha nzuri kwa mgonjwa kunampa matumaini ya kupata tiba nzuri katika maradhi  aliyonayo pindipo akitolewa maneno makali huchangia kumuadhiri kisaikolojia na kumkatisha tamaa”alisema Waziri.

Alisema sambamba na maadili katika kazi pia amewataka madaktari na wauguzi kuwa wazalendo katika ufanyaji wa kazi zao si tabia njema kuisambaza katika mitandao ya kijamii.

Alisema kwa upande wa Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya mnazi mmoja Madaktari  wameweza kujirekebisha na kutoa huduma iliyo bora kwa wagonjwa licha ya kuwa kunajitokeza baadhi ya vituo vya afya bado wanaitumia lugha chafu kwa wagonjwa .

Aidha alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma za matibabu  imefanya juhudi ya kujenga vituo vya afya katika sehemu tofauti ili mwananchi waweze kupata huduma hiyo kwa ukaribu.

Hata hivyo aliitaka jumuiya Madaktari Wanafunzi Tanzania kuengeza juhudi ya wataalamu kutokana na mahitaji yaliopo hivi sasa ya  teknolojia mpya za vifaa tiba zinahitaji watendaji wengi na wenye sifa za kuweza kuzitumia.

Alisema licha ya ununuzi mkubwa wa  mashine mpya za vifaa tiba pia kunaupungufu wa wataalamu katika hospitali za Zanzibar.

Nae Makamo ya Rais wa Jumuiya ya Madaktari Wanafunzi Tanzania  alisema lengo ni kuwasogezea wananchi huduma za afya iliyobora  na kuwafanyia uchunguzi wa maradhi mbalimbali ili waweze kupatiwa tiba kwa haraka pindipo wakigundulika mapema.

Alisema kuwapatia matibabu wananchi kutasaidia kupunguza kiwango cha maradhi kwa kupatiwa ushauri wa kidaktari mapema na kutasaidia watanzania  kufikia katika afya bora nchini

Aliweza kuzishukuru taasisi 17 zilizowaunga mkono kufanikisha zoezi la upimaji afya  ikiwemo wizara ya afya,

Zoezi hili la upimaji wa afya ni la  siku tatu ni la mara ya pili kufanyika Zanzibar awali lilifanyika mnamo mwaka  2014.

No comments:

Post a Comment

Adbox