Adbox

Saturday, October 26, 2019

TAKUKURU yabaini kikwazo urejeshwaji fedha za wakulima zilizoibiwa

Na Ahmad Mmow, Lindi.

Pamoja namafanikio yaliyopatikana kipindi kifupi kwa viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) kurejesha fedha za wakulima walizokwapua. Imebainika kwamba thamani ya mali za baadhi ya viongozi hazilingani na fedha walizoiba.

Hayo yameelezwa leo na mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa( TAKUKURU) wa mkoa wa Lindi, Steven Chami alipozungumza kwenye kikao cha tathimini ya ununuzi wa ufuta na maandalizi ya ununuzi wa korosho, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Lindi.

Chami alisema licha ya kurejeshwa takribani shilingi 300 milioni, taasisi hiyo imebaini kwamba mali baadhi ya viongozi  ambazo zimekamatwa na kupigwa picha thamani yake hailingani na fedha wanazodaiwa.

Alisema pamoja na changamoto huyo taasisi hiyo haitasinzia wala kulala hadi viongozi walioiba fedha za wakulima wa ufuta mkoani humu wamerejesha na wakulima wote wamelipwa. '' Tunataka hadi mwezi Desemba, mwaka huu(2019) viongozi wote walioiba fedha za wakulima wawe wamerejesha fedha zote,'' alisema Chami.

Mkuu huyo wa TAKUKURU wa mkoa wa Lindi alitaja baadhi ya mbinu zinatumika kuiba fedha
za wakulima ni watendaji na viongozi kuandika majina ya watu wengine tofauti na wakulima halisi kwenye stakabadhi za malipo na baadhi ya wanunuzi kuzidishiwa ufuta tofauti na malipo waliyofanya.

Chami alishangazwa na uwezo wa baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji kwakushindwa kuchukua hatua kuzuia utoroshwaji wa ufuta.

'' Nitoe wito, katika uchaguzi unaokuja tuchague viongozi waadilifu na waaminifu wenye uwezo wa kupambana na mambo kama haya,'' Chami alishauri.

Ofisa kiongozi huyo wa TAKUKURU wa mkoa wa Lindi alishangazwa na kitendo cha viongozi wanaotuhumiwa kuiba fedha kuendelea kuwepo madarakani. Huku ikijulikana kwamba wanadaiwa na wanatakiwa kurejesha fedha za wakulima.

Alionya kwamba kitendo hicho kitasababisha mapambano dhidi ya viongozi na watendaji wezi wa vyama vya ushirika yakose ufanisi na nguvu.

Kwaupande wake mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi licha ya kuagiza viongozi wa vyama ambao wanadaiwa fedha za wakulima wa ufuta na wanaotakiwa kurejesha wavuliwe nyazifa zao na  waondolewe madarakani. Alisema baadhi ya maofisa wa idara za ushirika sio waaminifu.

Alisema maofisa hao wamekuwa ni walimu wa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika kwa kuwafundisha njia na mbinu za kuiba fedha za wakulima.

No comments:

Post a Comment

Adbox