Adbox

Saturday, October 26, 2019

Dk. Shein aainisha China inavyosaidia Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amesema serikali itaendelea kuthamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Jamhuri ya Watu wa China sambamba na chama chake cha Kikomunisti cha CPC.

Alitoa kauli hiyo Ikulu mjini Zanzibar alipofanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CPC, Guo Yezhou. Dk Shein alisema ni vigumu kutaja maendeleo ya Zanzibar bila kuhusisha Jamhuri ya Watu wa China kupitia CPC kutokana na uhusiano na ushirikiano mwema na wa kihistoria.

Alisema serikali ya China imeifanyia mambo mengi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwamo Zanzibar kwa uungaji mkono katika kuimarisha sekta za maendeleo. Akitoa ushuhuda jinsi nchi hiyo ilivyoisaidia Zanzibar kuimarisha sekta za maendeleo, hususani afya, elimu, viwanda, kilimo, sekta ya habari, miundombinu, michezo, Rais Shein alisema China ni marafiki wa kweli kwani ilianza ushirikiano mara baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Alisema nchi hiyo imesaidia pia ujenzi wa kiwanda cha sukari Mahonda, Kiwanda cha sigara Maruhubi na kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kutoa nafasi nyingi za masomo nchini humo. Alieleza kuwa kubwa kuliko yote ni ukarabati mkubwa wa hospitali ya Abdalla Mzee mkoani Pemba na ukarabati wa uwanja wa Mao Zedong. Dk Shein alimweleza kiongozi huyo haja ya kukuza ushirikiano kati ya CCM na CPC pamoja na serikali ya Tanzania na China kama ulivyofanywa na waasisi wan chi hizo; Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong.

Alisema ushirikiano huo ulianza tangu mwanzo wa vyama vya ASP, TANU na hatimaye CCM. Alifafanua kuwa urafiki mzuri ulioneshwa na viongozi wa pande zote kwa kutembeleana jambo linalofanyika hadi sasa. Rais Shein alitumia fursa hiyo kushukuru serikali China kupitia CPC kusaidia ujenzi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kinachojengwa wilaya ya Kibaha mkoni Pwani.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CPC, Guo Yezhou alishukuru kwa mapokezi mazuri aliyopata pamoja na ujumbe wake tangu alipowasili nchini. Alisema miongoni mwa malengo ya ujio wake ni kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya China na Tanzania. Aliwasilisha salamu za Rais Xi Jinping kwa Rais Shein.

Naibu waziri huyo alimueleza Rais Shein kuwa chuo hicho cha uongozi cha Kibaha ni kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uongozi kwa nchi sita zenye vyama vya ukombozi vilivyoshirikiana na CPC ambavyo ni CCM, ANC, ZANU-PF, FRELIMO, MPLA na SWAPO.

Kiongozi huyo alimhakikishia Rais Shein kuwa China itaendelea kuunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo. Alipongeza miradi iliyokamilika huku akisisitiza kuwa nchi yake itaendelea kuisaidia Zanzibar kwa namna tofauti ikiwamo kuleta wataalamu hususani madaktari kutoka Jimbo la Jingsu.

No comments:

Post a Comment

Adbox