Serikali imeupongeza uongozi wa muda wa Jumuiya ya Wasindikaji Nafaka Tanzania (JUWANATA) kwa kukamilisha rasimu ya katiba ya umoja wao.
Pongezi hizo za serikali zimetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Masoko toka Wizara ya Kilimo Benito Kavenuka wakati wa mkutano maalum wa Juwanata uliofanyika Jijini Dar es Salaam .
Kavenuke amesema kuundwa kwa jumuiya ya wasindikaji mazao ya nafaka ni utekelezaji wa azimio la mkutano wa wafanyabiashara ya mazao ya nafaka uliofanyika mwezi Agosti mwaka huu chini ya Waziri wa Kilimo.
“Serikali inaunga mkono Juwanata kwa kutekeleza kwa haraka azimio la mkutano wa Waziri wa Kilimo na wafanyabiashara wa nafaka la kuanzisha jumuiya hii muhimu kwa ustawi wa viwanda vya mazao ya nafaka.” alisema Kavenuka.
Aliongeza kusema serikali itapenda kuona Viongozi wa jumuiya hii wanasimamia viwango vya ubora wa bidhaa za nafaka zinazalishwa ili kuwa na uhakika wa soko na bei nzuri.
Kavenuka amewataka pia kuongeza wigo wa kuwafikia wasindikaji waliopo mikoani kujiunga na jumuiya hii,ili serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo iwe rahisi kutoa huduma za kukuza sekta ya usindikaji nafaka nchini.
Akitoa taarifa ya mkutano huo maalum,Mwenyekiti wa muda wa Juwanata Oscar Munisi alisema lengo la jumuiya ni kuitikia kwa vitendo kauli mbiu ya serikali ya kujenga viwanda vya kuongeza thamani mazao ya nafaka .
Munisi aliongeza kusema jumuiya yao inaundwa na wanachama wamiliki wa viwanda vya kusindika nafaka na mafuta toka mikoa yote ya Tanzania bara ambapo kazi ya kuandaa katiba ya muda ilishirikisha wadau wote
“Tunataka kuwa na Katiba itakayosaidia kusajili wasindikaji wote nchini hususan wajasiliamali wadogo ili tuwe na sauti ya pamoja katika kuyafikia masoko ya bidhaa za nafaka kwa ushirikiano na serikali” alisema Munisi
Alitaja changamoto ya wajasiliamali wasindikaji kwa sasa nchini kuwa ni kufikia masoko kama ya Lubumbashi Kongo imekuwa ngumu kwa kukosekana chombo cha kuwaratibu.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Baraza la Nafaka la Afrika Mashariki (EAGC) Ikunda Terry amewataka wasindikaji hususan wa mchele kuongeza ubora ili kufikia soko kubwa la nchi za Uarabuni.
“Tanzania ina fursa ya soko la uhakika la mchele kwani sasa uzalishaji umefikia tani 2,200,000 wakati matumizi ya ndani kwa mwaka ni kama tani milioni moja,kwa hiyo tunayo ziada ya zaidi ya tani milioni moja kwa ajili ya kuuza nje ya nchi” alisisitiza Ikunda.
Kufanyika kwa mkutano huu maalum kunafatia mkutano wa Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga alioitisha hapo tarehe 29 na 30 Agosti mwaka huu kujadili changamoto za masoko ya mazao ya nafaka nchini.
Thursday, October 31, 2019
Serikali yapongeza Juwanata kwa kuanzisha Jumuiya ya wasindikaji Nafaka
Tags
# Top News
About Sultan Mapigo
SULTAN MAPIGO: Kuwa wa kwanza kuhabarika, Tafadhari usisahau kusubscribe kushare na kucomment
Top News
Tags:
Top News
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment