Adbox

Monday, October 28, 2019

Rais Magufuli apokea hati za utambulisho wa Mabalozi

Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli apokea hati za utambulisho za Mabalozi wa Umoja wa Ulaya, Finland na Rwanda. Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 28 Oktoba, 2019 amepokea hati za utambulisho za Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) hapa nchini Mhe. Manfred Fanti, Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Riitta Swan na Balozi wa Rwanda hapa nchini Mhe. Mej. Jen. Charles Karamba, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mhe. Rais Magufuli baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho Mhe. Balozi Manfred Fanti ameishukuru Tanzania kwa kumpokea kuja kuiwakilisha EU hapa nchini na amesema katika kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano na EU na Tanzania atajielekeza zaidi katika masuala ya maendeleo kwa kuwa anaamini kuna mambo mengi na mazuri ya kufanya yatakayoiwezesha Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kama ilivyopanga.

Mhe. Balozi Fanti ameongeza kuwa anaamini katika mazungumzo ya pamoja kati ya Tanzania na EU katika masuala mbalimbali na kwamba katika kipindi chake anatarajia kutilia mkazo miradi ya kuzalisha nishati ya umeme kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na utekelezaji wa miradi mingine iliyopo katika makubaliano ya 11 ya mkataba wa mfuko wa maendeleo ya EU uliotengewa shilingi Trilioni 1.583 yanatekelezwa.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Balozi Fanti kwa msimamo wake wa kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na EU na amesema Tanzania inatambua uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na EU na kwamba ipo tayari kushirikiana na Balozi huyo katika utekelezaji wa masuala yenye maslahi kwa pande zote mbili.

Kwa upande wake Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Riitta Swan pamoja na kushukuru kwa kupokelewa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa mafanikio makubwa katika kupambana na rushwa na amesema katika kipindi chake hapa nchini atahakikisha maeneo ya uhusiano kati ya Tanzania na Finland yanaimarishwa ikiwemo mradi wa utunzaji wa mazingira, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na utawala bora.

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru kwa dhamira yake ya kukuza zaidi ushirikiano na uhusiano na Tanzania na amesema Tanzania itakuwa tayari kutoa ushirikiano wowote atakaouhitaji.

Nae Balozi wa Rwanda hapa nchini Mhe. Mej. Jen. Charles Karamba ameishukuru Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Adbox